Sunday, 5 April 2015

Morocco ruksa kushiriki Mataifa ya Afrika 2017/19



CAIRO, Misri
SHIRIKISHO la Soka la Afrika (CAF) limethibitisha leo Jumapili kuwa, Morocco itashiriki mechi za kufuzu kwa ajili ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika za mwaka 2017.

Alhamisi Mahakama ya Usuluhishi wa Mambo ya Michezo (CAS) ilitengua adhabu ya CAF ya kuifungia Morocco kushiriki fainali mbili za Mataifa ya Afrika za mwaka 2017 na 2019.

Lakini Ijumaa; Mkurugenzi wa Mawasiliano wa CAF Junior Binyam alisema: "Kuna vikao vingi vya kufanyika kabla ya suala hili kufikia hatma yake.

"Acha tuone nini kitatokea. Ratiba inatakiwa kupangwa Aprili 8."

Leo Jumapili, Shirikisho la Soka la Afrika lilitangaza kukubali uamuzi uliotolewa na CAS baada ya kikao chake cha Kamati ya Utendaji, na kutoa sababu katika mtandao wa shirikisho hilo.

Morocco ilifungiwa kushiriki fainali mbili za Mataifa ya Afrika baada ya dakika za mwisho kushindwa kuandaa fainali za mwaka huu za mashindano hayo kwa madai ya kuhofia kuenea kwa ugonjwa wa Ebola barani Afrika.

Shirikisho la Soka la Morocco (FRMF) liliiomba CAF kuahirisha fainali hizo, lakini ombi lake lilikataliwa na badala yake fainali hizo zilihamishiwa Guinea ya Ikweta, na Morocco iliondolewa katika mashindano hayo.

No comments:

Post a Comment