*Waunda Kamati ya Kufanya Mabadiliko ya Katiba
KAMATI ya Utendaji ya Chama cha Waandishi wa
Habari za Michezo Tanzania (TASWA) ilikutana hivi karibuni na kujadili masuala
mbalimbali.
A ; Katiba ya TASWA
Kamati ya Utendaji ya TASWA imemteua
Mwenyekiti wa zamani wa TASWA, Boniface Wambura kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya
Kusimamia Mabadiliko ya Katiba ya TASWA.
Wambura alikuwa Mwenyekiti wa TASWA kuanzia
Februari mwaka 2004 hadi Agosti 2010, pia amepata kukaimu nafasi ya Uenyekiti
wa TASWA kuanzia mwaka 2003 hadi Uchaguzi Mkuu ulipofanyika mwaka 2004. Kwa
sasa Wambura ni Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
TASWA inatambua Wambura licha ya kuwa na
taaluma ya uandishi wa habari, ni mwanasheria, hivyo inaamini uzoefu wake ndani
ya TASWA pamoja na TFF ambako amewahi kuwa Katibu wa Kamati ya Mabadiliko ya
Katiba ya shirikisho hilo utasaidia sana kupata katiba nzuri.
Wajumbe wengine wa kamati hiyo yenye jumla ya
watu watano ni Mhadhiri Msaidizi wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na
Mawasiliano Kwa Umma (SJMC) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Egbert
Mkoko.
Mkoko kwa sasa ni Makamu Mwenyekiti wa TASWA.
Wengine ni Mhariri wa habari za michezo wa gazeti la Daily News, Nasongelya Kilyinga
na Mtendaji Mkuu wa Bin Zubeiry Blogspot, Mahmoud Zubeiry, ambaye amepata kuwa
Mhariri wa habari za michezo wa magazeti mbalimbali nchini.
Mwingine ni mtangazaji wa zamani wa Redio
Tumaini Dar es Salaam, ambaye kwa sasa ni mfanyakazi wa Shirika la Nyumba la
Taifa (NHC) kitengo cha huduma kwa wateja, Domina Rwemanyila. Wajumbe wote ni
wanachama wa TASWA.
Nia ya TASWA ni kamati hiyo ifanye kazi ndani ya siku 90 ili Rasimu ya Katiba
ijadiliwe katika Mkutano Mkuu wa TASWA unaotarajiwa kufanyika Julai 25 na 26
mwaka huu mkoani Morogoro.
B; Media Day
Kila mwaka TASWA imekuwa ikiandaa tamasha
maalum kwa ajili ya wafanyakazi mbalimbali wa vyombo vya habari (Media Day
Bonanza), ambapo mwaka jana halikufanyika kutokana na sababu mbalimbali.
Mwaka
huu TASWA imepanga bonanza hilo lishirikishe wadau 2,000 kutoka vyombo
mbalimbali vya habari na tayari kampuni mbili zimejitokeza kutaka kudhamini
bonanza hilo, lakini si kwa kiwango ambacho chama kinataka.
Kutokana na hali hiyo mazungumzo bado
yanaendelea na wadhamini hao wametoa masharti ya kupunguza idadi ya washiriki
kutoka 2,000 waliopendekezwa na chama hadi kufikia 500, idadi ambayo kwa uzoefu
wetu ni ndogo na kwa kadri watu walivyo na hamu ya kujumuika pamoja inaweza
isikate kiu ya wanahabari na italeta malalamiko kwa watakaokosa.
Nia ya TASWA ni kuwaweka pamoja waandishi wa
habari za afya, siasa, uchumi, michezo, mazingira na nyinginezo pamoja na
wafanyakazi wa vyombo mbalimbali kujadili masuala yanayowahusu na kisha
kuburudika kwa pamoja.
Kutokana na hali hiyo TASWA imekubaliana na
wadhamini hao, watafutwe wadhamini wengine waongeze nguvu na kufanya bonanza
hilo liwe la aina yake na tuna imani katika wiki chache zijazo suala la Media
Day litakuwa limekamilika.
Kwa mazingira hayo Kamati ya Utendaji katika
kurahisisha jambo hilo, imeunda kamati maalaum ambayo Mwenyekiti wa TASWA FC,
Majuto Omary atakuwa ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Media Day na
Katibu wake atakuwa Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando.
C; Mafunzo
Kama tulivyopatangaza mwezi uliopita, TASWA
inaendelea na programu za mafunzo kwa waandishi wa habari za michezo, ambapo
awamu ya kwanza ilifanyika Machi 25 mwaka huu na kuhusisha washiriki 40, ambapo
30 walikuwa chipukizi na 10 wa kada ya kati.
Awamu nyingine mbili zinatarajiwa kufanyika
mwezi ujao, ambapo awamu ya kwanza itakuwa Dar es Salaam mapema mwezi ujao
ikihusisha washiriki 40 kati yao 30 ni wa kada ya kati na 10 wakiwa waandishi
wazoefu. Awamu ya pili itafanyika mwishoni mwa mwezi huo.
Nawasilisha,
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
22/04/2015
0717-665544
No comments:
Post a Comment