Mwenyekiti wa Chama cha Netiboli Tanzania Chaneta), Annie Kibira wakati wa mkutano mkuu wa TOC leo katika Kituo cha Amani Welezo, Zanzibar. |
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
TIMU ya Jeshi Stars imejitoa kushiriki mashindano ya netiboli ya
Muungano yanayotarajia kuanza Jumanne Desemba 15 kwenye Uwanja wa Gymkhana mjini Zanzibar.
Jeshi Stars ni miongoni mwa timu za Tanzania Bara zilizothibitisha
kushiriki mashindano hayo kabla ya kujitoa katika dakika za mwisho kabisa za
mashindano hayo.
Timu zingine za Bara zitakazoshiriki mashindano hayo ni pamoja na
mabingwa Uhamiaji, JKT Mbweni, Polisi, Tumbaku ya Morogoro, Mbeya City ya
Mbeya.
Mwenyekiti wa Chama cha Netiboli Tanzania Chaneta), Annie Kibira
alisema jana mjini hapa, ambako anahudhuria mkutano mkuu wa Kamati ya Olimpiki
Tanzania (TOC) kuwa, alipewa taarifa juzi kuwa Jeshi Stars wamejitoa katika
mashindano hayo.
Alisema kuwa anasubiri barua yao ili kujua sababu kamili
iliyopelekea kujiondoa katika dakika za mwisho katika mashindano hayo.
Hatahivyo, taarifa zingine zinasema kuwa, timu hiyo imejiondoa
baada ya baadhi ya wachezaji wake kwenda katika kozi ya kikazi.
Timu za Zanzibar zitakazoshiriki mashindano hayo ni JKU, Mafunzo,
KBZ, Zimamoto, Chake Stars na Wete Stars.
Wakati
huohuo, timu za Uhamiaji na JKT Mbweni zinatarajia kutua leo mjini hapa
kwa ajili ya mashindano hayo.
No comments:
Post a Comment