Mwanariadha Nuru Kombo ameibuka kidedea kwa kutwaa medali
mbili za dhahabu kwenye mbio za mita 100 na 200 katika mashindano ya Filbert
Bayi Schools Inter Houses Sports Bonanza.
Mashindano hayo ya siku mbili yalianza Juzi Jumatano kwenye
viwanja vya Filbert Bayi Kibaha Mkuza mkoani Pwani.
Katika mbio za mita 100, Nuru alikimbia kwa sekunde 16:13 na
kuwapiku Shyrose Christopher aliyemaliza wa pili akikimbia kwa sekunde 17:03 na
Khadija Issa aliyekimbia kwa sekunde 18:59.
Kwenye mbio za mita 200, Nuru tena alitwaa dhahabu akikimbia
kwa sekunde 36:24 na kuwapiku Shyrose aliyemaliza wa pili akikimbia kwa sekunde
36:91 na Khadija aliyemaliza wa tatu akikimbia kwa sekunde 37:29.
"Napenda riadha, nimekuwa nikijifua mara kwa mara na
nina ndoto ya kuja kuwa msomi na mwanariadha nyota wa kimataifa baadae," alisema Nuru ambaye ni
mwanafunzi wa sekondari wa Shule ya Filbert Bayi.
Katika mbio za mita 400, Hidaya Jongo aliibuka kidedea
akikimbia kwa dakika 1:20:86 huku Salome Edger akimaliza kwenye nafasi ya pili
baada ya kukimbia kwa 1:22:31 na Nuru akaambulia medali ya tatu akikimbia kwa
dakika 1:27:01.
Upande wa wavulana, Benson Mlacha aliibuka kinara akikimbia
kwa dakika 1:03:97 huku Twalibu Abdallah aliyekimbia kwa dakika 1:04:21 na Amos
Leonard aliyekimbia kwa dakika 1:04:56 wakitwaa medali ya fedha na shaba.
Kwenye mbio za mita 200, Abdallah Fauz aliibuka kinara
akikimbia kwa sekunde 28:81 na kuwapiku Valentino Peter aliyekimbia kwa sekunde
29:63 na Henry Sebastian aliyekimbia kwa sekunde 29:82 na kumaliza kwenye
nafasi ya pili na tatu.
Kwenye mbio za mita 100, Stanley Benson aliibuka kidedea
akikimbia kwa sekunde 11:89 na Faris Jaffu alimaliza wa pili akikimbia kwa
sekunde 12:01 na Clement Mgaya alihitimisha tatu bora akitumia sekunde 14:22
kumaliza mbio.
Mwenyekiti wa FBF, Filbert Bayi alisema katika mashindano
hayo ya siku mbili wanafunzi wa shule hizo walichuana kwenye soka, netiboli na
riadha.
"Michezo ni sehemu ya ukuaji mzuri kwa watoto, pia
inawaongezea uelewa mzuri, hivyo shule zetu zimekuwa na siku maalumu ya michezo
kila mwaka," alisema Bayi ambaye anashikilia rekodi ya Jumuiya ya Madola ya mbio za meta 1500, ambayo haijavunjwa kwa miaka 44 sasa.
NB:Matokeo ya Jumla ya bonanza hilo yatafuata baadae.
NB:Matokeo ya Jumla ya bonanza hilo yatafuata baadae.
No comments:
Post a Comment