Wednesday, 9 May 2018

Rotary Club Kuandaa Mbio za Mbuzi 2018

Rais wa Klabu ya Rotary Dar es Salaam, Oysterbay, Anne Saels (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kutangaza dhumuni la klabu hiyo kuendeleza mashindano ya mbio za mbuzi kwa mwaka 2018. Chini ya chapa mpya ya ‘The Rotary Goat Races’. Kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya mbio za mbuzi,  Amish Shah.
Na Mwandishi Wetu
MASHINDANO ya mbio za mbuzi mwaka huu yanatarajia kufanyika Juni 23 kwenye viwanja vya The Green Oysterbay jijini Dar esSalaam,imeelezwa.

Mbio hizo zinafanyika chini ya muandaaji mpya, ambaye ni Klabu ya Rotary ya Dar es Salaam Oysterbay baada ya muandaaji wa awali kusitisha shughuli hiyo baada ya kuiandaa kwa takribani miaka 17.
Methew Hellela; Mkuu wa Kamati ya Maandalizi ya Mbio za Mbuzi 2018 akizungumza wakati wa uzinduzi wa nembo mpya ya mbio hizo leo. Kushoto ni Rais wa Rotary Dar es Salaam, Oysterbay, Anne Saeels na kulia ni Mjumbe wa Bodi ya Mbio za Mbuzi, Amish Shah.
Rais wa Rotary Dar es Salaam Oysterbay, Anne Saeels  alisema jana kuwa, waandaaji wapya wataendelea na utaratibu ule ule wa kuendesha mashindano hayo kama ilivyokuwa huko nyuma.

Alisema kuwa tofauti na miaka ya nyuma, mapato yote yatakayotokana na mashindano ya mwaka huu, hayatapelekwa katika mashirika mbalimbali yanayopokea misaada na badala yake fedha hizo zitatumika kwa ajili ya miradi binafsi ya hutoaji huduma ya klabu ya Rotary Dar es Salaam Oysterbay.
Mjumbe wa Bodi ya Mbio za Mbuzi za Rotary 2018, Amish Shah akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam kuhusu mbio hizo. Kushoto ni Rais wa Rotary Dar es Salaam, Oysterbay Anne Saels na kulia ni Mkuu wa Kamati ya Maandalizi ya mbio hizo, Methew Hellela.
Alisema miradi hiyo itazingatia hasa masuala mbalimbali ya elimu kwa manufaa ya jamii.

“Tunaamini kwamba kupitia miradi ya elimu iliyopangwa tunaweza kuleta tofauti kubwa kwenye maisha ya watu katika jamii na tunafuraha mashindano yam bio za mbuzi ya Rotary yatakuwa na jukumu katika kukamilisha hili, “alisema Saels.

Naye mwenyekiti wa Bodi ya Mbio za Mbuzi za Rotary, Amish Shah alisema kuwa anaamini mashindano hayo yatakuwa mazuri sana na hayatawaangusha mashabiki, ambapo anaamini yatavutia mashabiki wengi.
Rais wa Rotary Club Dar es Salaam, Oysterbay, Anne Saels akifurahia jambo na mwenyekiti wa Bodi ya Mbio za Mbuzi 2018, Amish Shah wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo. 
Alisema kuwa mashindano hayo mwaka huu yamedhaminiwa na Coca Cola, Toyota na Swiss International Airlines.

Alisema kuwa ni matarajio yao kuwa huo ni mwanzo na anaamini kuwa kila mwaka watajitahidi kuhakikisha mashindano hayo yanafanyika tena kwa ufanisi wa hali ya juu na kuvutia watu wengi.
Mwenyekiti wa Bodi ya mbio za mbuzi za Rotary, Amish Shah  akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam wakati wa kutangaza mbio hizo zitakazofanyika Juni 23. Katikati ni Rais wa Klabu ya Rotary Dar es Salaam, Oysterbay, Anne Saels na Mkuu wa Kamati ya Maandalizi, Abdulrahman Hussein .

No comments:

Post a Comment