Na Mwandishi Wetu, Dodoma
BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jana
lilipuka kwa shangwe baada ya mabingwa wapya wa soka kutinga katika chombo
hicho cha kutunga sheria nchini.
Shangwe hizo zililipuka baada ya Mwenyekiti wa Bunge,
Najma Giga kutangaza kwamba timu hiyo imekuja bungeni kutembelea, hali iliyofanya wabunge kushindwa
kujizuia na kuinuka kwenye viti huku wakishangilia, wengi wao wakionesha vitabu
vya bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, ambavyo vilikuwa vya
rangi nyekundu.
Hali hiyo ilitokea baada ya kipindi cha maswali na
majibu na iliwachukua wabunge takriban dakika tatu kushindwa kuficha hisia zako
na kushangilia na wengi wao wakisema ‘This is Simba’, msemo ambao umekuw
ukisemwa na msemaji wa klabu hiyo,
Haji Manara na sasa umekuwa maarufu zaidi
kwa mashabiki wa timu hiyo.
Miongoni mwa wabunge walionogesha bunge ni Mbunge wa
Lushoto, Shaaban Shekilindi (CCM) ambaye alionesha fulana jezi ya Simba
iliyoandikwa ‘Simba Bingwa 2018-2019, huku
akiizungusha na kuzidisha shangwe, huku Mbunge wa Mbozi, Pascal Haonga(Chadema)
alionesha juu tai nyekundu.
Awali, akikaribisha timu hiyo, Giga alisema timu hiyo
imekuja na viongozi 10 na wachezaji 48 na kuwataja viongozi hao kwa majina
wakiwemo Salim Abdallah, Aden Rage, Mohamed Dewji, Idi Kajuna, Haji Manara,
Richard, Kocha Pierre, Masoud Juma na mwisho akamtambilisha Emmanuel Okwi na
kuufanya ukumbi wa bunge kulipuka ingawa wapo waliomkosoa kwa kutosimama kama
wenzake walivyokuwa wakitambulishwa.
Okwi ndiye mfungaji bora hadi sasa wakati ligi hiyo
ikielekea ukingoni.
Mara baada ya wachezaji hao kusimama Wabunge walianza
kushangilia huku baadhi wakipiga makofi na viti kuonesha kufurahishwa na ujio
wa timu hiyo ambapo Giga aliingilia “Waheshimiwa,Waheshimiwa Wabunge naomba
tusikilizane naamini kabisa vifijo hivi vimesaidiwa na Wabunge ,mashabiki wa
Yanga kwa vile ni waungwana”.
Kabla ya timu hiyo kutambulishwa, wabunge wakati
wakiuliza maswali na mawaziri kujibu wengi walikuwa wakieleza furaha yao kwa
timu hiyo kunyakua ubingwa.
No comments:
Post a Comment