Na Mwandishi
Wetu
VIGOGO vya soka
Tanzania, Simba na Yanga vitamenyana Julai 5, mwaka huu katika mechi ya Kundi C
ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Kagame Cup, inayotarajiwa
kuanza Juni 28 hadi Julai 13 mwaka huu Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa
Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati, Cecafa, Nicholas Musonye alisema leo kuwa mbali na Simba
na Yanga, timu nyingine katika Kundi hilo ni pamoja na Dakadaha ya Somalia na
Saint George ya Ethiopia.
Musonye alisema
kwamba Kundi A linaundwa na timu za Azam FC, KCCA ya Uganda, JKU ya Zanzibar na
Kator FC ya Sudan Kusini, wakati Kundi B linaundwa na timu za Rayon Sports ya
Rwanda, Gor Mahia ya Kenya, Lydia Ludic ya Burundi na Ports ya Djibouti.
Musonye
aliishukuru Tanzania kwa kukubali kuwa wenyeji wa michuano hiyo na akasema
kwamba anatarajia itafana kwa sababu ya rekodi ya nchi hii kuandaa mashindano
yalioyokuwa na msisimko mkubwa miaka ya nyuma.
Musonye ambaye
alisema mashindano yatafanyika viwanja vya Taifa na Azam Complex, Chamazi – pia
amewapongeza Rwanda na Rais wao, Paul Kagame kwa kuwa wadhamini wa mashindano
haya kwa zaidi ya miongo miwili sasa.
Musonye alisema
kuwa wamelazimika kufanya mashindano ya mwaka huu sambamba na Fainali za Kombe
la Dunia nchini Urusi, kwa sababu wasipofanya mwezi huu hayatafanyika tena kwa
mwaka wa tatu mfululizo.
Hata hivyo,
Musonye alisema kuwa watatoa ratiba nzuri ambayo haitaruhusu mashindano ya
mwaka huu kuingiliana na mechi za Kombe la Dunia.
Kwa upande
wake, Mtendaji Mkuu wa Azam Media Limited, Tido Mhando alisema kwamba wataitumia michuano hiyo kukizindua kituo chao
Radio, Uhai FM na akahakikishia kwamba pamoja na mashindano hayo kufanyika
sambamba na Kombe la Dunia, lakini yatafana tu.
FIFA imeridhia
Kagame kufanyika mwezi huu tofauti na agizo lake la kutotaka katika mwezi wa
Fainali za Kombe la Dunia yasifanyike mashindano mengine yoyote, kwa sababu
washiriki watano wa michuano hiyo wapo kwenye hatua ya makundi ya michuano ya
Afrika, ambayo kwa sasa imesimama kupisha Kombe la Dunia, itarejea Julai baada
ya kumalizika kwa michuano hiyo nchini Urusi.
Hao ni KCCA ya
Uganda iliyopo Kundi A katika Ligi ya Mabingwa Afrika na nyingine nne kwenye
Kombe la Shirikisho, ambazo ni Gor Mahia ya Kenya, Rayon Sports ya Rwanda,
Yanga ya Tanzania zilizopo Kundi D zote na Al-Hilal ya Sudan iliyopo Kundi A.
Na kwa sababu
hatua ya makundi ya michuano hiyo ya Afrika itakwenda hadi Agosti, mwezi ambao
msimu mpya wa Ligi Kuu nyingi duniani huanza – michuano ya Kagame isipofanyika
mwezi huu kuna hatari isifanyike tena na mwaka huu kwa mara ya tatu mfululizo.
Azam FC ndiyo
mabingwa wa mwisho wa michuano hiyo ilipofanyika Tanzania, walipowafunga Gor
Mahia 2-0 katika fainali Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, mabao ya
waliokuwa washambuliaji wake hatari, John Raphael Bocco dakika ya 17 na Muivory
Coast, Kipre Herman Tchetche dakika ya 64.
Na hiyo ndiyo
ilikuwa michuano iliyomtoa mshambuliaji Mkenya, Michael Olunga ambaye kwa sasa
anachezea Girona FC ya Hispania kwa mkopo kutoka Guizhou Zhicheng ya China.
Baada ya
kufungha mabao matano akiwa na Gor Mahia na kuibuka mfungaji bora akiwapiku ,
Osman Bilal Salaheldin wa Al-Khartoum ya Sudan aliyefunga mabao manne sawa na
Tchetche wa Azam FC, Olunga akachukuliwa na Djurgardens IF ya Sweden mwaka 2016
iliyomuuza Guizhou Zhicheng mwaka 2017.
Na Tanzania
itawakilishwa na Azam FC kama mabingwa watetezi wa mashindano na Yanga SC, kama
mabingwa wa nchi.
No comments:
Post a Comment