Friday, 4 May 2018

NMB Yakabidhi Jeshi Vifaa vya Michezo vya Mil 10


Mlezi wa timu za Jeshi, Luten Kanal, David Mziray akipokea vifaa vua michezo kutoka kwa Meneja Mwandamizi wa NMB, Mahususi kwa wateja, Gibson  Mlaseko kwa ajili ya michezo ya Mkuu wa Majeshi itakayofanyika jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu
BENKI ya NMB leo imetoa vifaa vyenye thamani ya Sh milioni 10 kwa timu za Majeshi, ambazo zinajiandaa na mashindano ya Majeshi yanayotarajia kuanza Mei 8 hadi 20, mwaka huu kwenye viwanja vya Uhuru na Twalipo Jijini Dar es Salaam.

Michezo mbalimbali ikiwemo soka, netiboli, riadha, ngumi, kulenga shaba, mpira wa mikono inatarajiwa kuwepo na washindi watazawadiwa zawadi mbalimbali.

Akizungumza kwenye hafla ya kukabidhia vifaa hivyo Makao Makuu ya Meneja Mwandamizi na mahusiano kwa wateja wa NMB, Gibson Mlaseko alisema kuwa sababu ya kutoa msaada huo ni kutokana na mahusiano mazuri waliyokuwa nayo na JWTZ, katika mambo ya michezo.

“Nashukuru kwa mahusiano mazuri kati yetu na JWTZ kwani hii ni mara ya tatu tunasaidiana nao katika maswala mbalimbali ya michezo, pia lengo la msaada huu ni kutambua umuhimu wa michezo kuwa ni kuibua vipaji kujenga Afya na ajira hivyo tuna imani wenzetu watavitumia vifaa hivi vizuri na kufikia malengo,” alisema Mlaseko.

Kwa upande wake, Luteni Kanali David Mziray aliishukuru NMB, kwa msaada huo na kusema watahakikisha wanavitumia vizuri ili kutimiza malengo ambayo wamejiwekea katika mashindano hayo.

“Tunawashukuru NMB kwa msaada huu vifaa hivi vitaongeza chachu ya mashindano yetu ambayo hufanyika kila mwaka tunaomba na kampuni zingine ziige mfano wao ili kuinua michezo nchini,” alisema Mziray.

Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na mipira ya michezo yote, Jezi za michezo yote, michezo mingine ambayo itashindaniwa katika michuano hiyo ambayo hufanyika kila mwaka.

No comments:

Post a Comment