Wednesday, 30 August 2017

Waziri aridhishwa na kasi ya ujenzi Terminal 3

Mkurugenzi wa mradi wa jengo la tatu la abiria la Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Wolfgang Marschick (kushoto) akiwa na  Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Prof. Makame Mbarawa (wa pili kushoto) akikagua mradi wa jengo hilo. Kulia ni Meneja wa Mradi, Ray Blumrida.
 Na Mwandishi Wetu
UJENZI wa sehemu ya tatu (Terminal Three) ya Kiwanja cha Ndege cha Julius Nyerere (JNIA) unatarajia kukamilika Oktoba mwakani.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof Makame Mbarawa alithibitisha hilo mara baada ya kukamilisha ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa eneo hilo  kiwanja hicho.

Alisema kuwa ujenzi wa Terminal 3 hadi sasa umekamilika kwa asilinia 64, ambapo alisema mkandarasi anaendelea vizuri na Serikali haidaiwi chochote.

Alisema Serikali imefanya malipo yote kwa wakati, ambapo aliongeza kuwa wamefanya hivyo ili kuhakikisha kila kitu kinafanyika kama kilivyopangwa ili sehemu hiyo ianze kutumika rasmi Oktoba mwakani.

Alisisitiza kuwa sehemu hiyo inatarajia kuchukua kwa wakati mmoja ndege 20 za airbus, huku kukiwa na madaraja 20 ya kupandia na kutokea katika ndege.

Alingeza kusema kuwa zaidi ya abiria milioni 8 wanatarajia kupitia sehemu hiyo kwa mwaka, ikiwa ni kama mara nne ukilinganisha na idadi inayohudumiwa sasa katika Terminal Two.

Mbali na kodi na fedha za kigeni nchini, Prof Mbarawa alisema kuwa Tanzania itafaidika kwa kuongezeka kwa ajira na mambo mengine.

Alikiri kuwa Terminal Two ambayo inatumika sasa inakabiliwa na changamoto nyingi, na ndio sababu Serikali imeamua kutumia fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi huo.

Alipoulizwa hadi sasa Serikali imetumia kiasi gani cha fedha kwa ujenzi huo, waziri alisema kwa sasa hana kiasi kamili kwa sababu fedha zimekuwa zikitolewa kwa awamu, lakini wananchi wanatakiwa kujua kuwa mradi huo utagharimu sio chini ya bil 560.
“Kufuatia maendeleo mazuri ya ujenzi wa mradi huo Serikali inaangalia uwezekano wa kutoa zabuni kwa ajili ya kampuni za mizigo.

Kwa sasa, waziri alisema kuna kampuni mbili tu za kushughulikia mizigo, ambazo ni Swiss-Port na Nas Dar Airco, ambapo kampuni zaidi zinatakiwa ili kukidhi mahitaji ya abiria.
 “Uwepo wa kampuni nyingi za kushughulikia mizigo kutasaidia kuwepo kwa huduma bora kwani kila moja itataka kushinda na mwenzake iki kupata wateja wengi, “alisema.




Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof Makame Mbarawa akiagana na Mkurugenzi wa Mradi wa Jemgo la Tatu la Kiwanja cha Kimataifa cha Ndege cha Julius Nyerere (JNIA), Wolfgang Marschick baada ya waziri kumaliza ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa mradi huo. 

No comments:

Post a Comment