Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege (TAA) imesema itafunga mitambo
ya kubaini watu waliomeza dawa za kulevya katika jengo la abiria namba tatu
(Terminal III) kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Hatua hiyo ni katika kupambana na tatizo la dawa za kulevya
na kuhakikisha hakuna dawa zinazopitishwa kupitia uwanja huo.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, Salim Msangi (kushoto) akielezea jambo wakati wa ziara ya wajumbe wa Kamati ya Ardhi na Mawasiliano ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar |
Msangi alisema, mbali na mtambo huo kufungwa katika kiwanja
huo ili kuhakikisha hakuna dawa zinazopitishwa lakini pia taasisi nyingine
mbalimbali ikiwemo za madini zitakuwa na nafasi katika uwanja huo ili kuhakikisha
hakuna madini yanayotoroshwa kwenda nje ya nchi.
"Ni jengo la aina yake kwa kweli, kwa sababu tunataka
Airport ya Dar es Salaam iwe ni kiunganishi cha kwenda sehemu nyingine lakini
pia kwa kuwa tunafufua shirika letu la ndege iwe ni sehemu ambapo safari
zinaanzia hapa na kwenda kuchukua watu katika nchi mbalimbali na kuwaleta
hapa," alisema.
Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar wakitembelea Kiwanja cha Kimataifa cha Ndege cha Julius Nyerere (JNIA) Terminal 3 leo jijini Dar es Salaam.
|
Msangi alisema, hatua hiyo itasaidia kuongeza fedha za kigeni
na mapato kwani ndege zilizonunuliwa na serikali zitaweza kwenda katika nchi
mbalimbali na hivyo kuleta watalii nchini.
Aidha, alisema sambamba na mradi huo pia wana mpango wa
kujenga hoteli ya kisasa karibu na uwanja huo ili kuwarahisishia abiria na
wageni ambao wanapenda kukaa karibu na uwanja wa ndege.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na
Usafirishaji wa Zanzibar, Mohamed Ahmed Salim alisema, kupitia ziara hiyo
wamejifunza mambo mengi ambayo wataenda kuangalia namna ya kuyaweka katika
mradi wa ujenzi wa jengo la abiria namba mbili (Terminal II) katika Uwanja wa
Ndege wa Zanzibar.
Alisema mradi huo awali ulikwama kutokana na changamoto
mbalimbali lakini kwa sasa wameshafikia muafaka na kwamba ujenzi utaanza muda
wowote kuanzia sasa na utachukua miezi 18.
"Kwa mwaka jana uwanja ule umehudumia wageni miliomni
moja, tulikuwa tunalenga kujenga jengo litakalohudumia abiria milioni moja
nukta mbili lakini kwa kuangalia idadi ya watalii inavyoongeza na dira ya
maendeleo tukasema ni bora jengo la kuhudumia abiria milioni moja nukta
sita," alisema Salum.
Alisema hatua hiyo ilisababisha kuchelewa kuanza kwa ujenzi
kwa kuwa walikuwa kwenye majadiliano ya wafadhili wa mradi huo ambao ni China
kupitia Benki ya Exim China.
Naye Mwenyekiti wa kamati hiyo, Hamza Hassan Juma alipongeza
maendeleo ya ujenzi huo pia kupongeza hatua ya serikali kujenga awamu ya pili
kwa kutumia fedha za ndani.
"Hii ni nzuri sana, kwasababu inaonesha kuna mambo
tunaweza sisi wenyewe, bila kutegemea misaada. Pia tumejifunza mengi tukirudi
Zanzibar tutaishauri serikali," alisema Juma.
No comments:
Post a Comment