Na Mwandishi Wetu
MCHEZO wa kirafiki kati ya Yanga na Singida United uliopangwa
kufanyika Agosti 6, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam umerudishwa nyuma
kwa siku moja kupisha shughuli maalum ya Kiserikali siku hiyo na sasa
utafanyika Jumamosi ya Agosti 5.
Yanga inatarajiwa kumenyana na Singida United
inayofundishwa na kocha wake wa zamani, Mholanzi Hans van der Pluijm katika
mchezo maalum wa kila timu kujaribu kikosi chake kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu
ya Tanzania Bara.
Na kwa sasa kikosi cha kocha Mzambia, George Lwandamina kipo
mjini Morogoro kimeweka kambi ya kujiandaa na msimu mpya, wakianza na mchezo wa
Ngao ya Jamii, dhidi ya mahasimu, Simba, Agosti 23, mwaka huu Uwanja wa Taifa.
Singida United imerejea Ligi Kuu msimu huu tangu iliposhuka mwaka
2002, lakini baada ya kupanda imefanya usajili wa gharama kubwa, ikichukua
wachezaji wenye uzoefu mkubwa kutoka timu mbalimbali za ndani na nje ya nchi.
Timu hiyo si tu itatoa upinzani kwa Yanga Agosri
5, bali pia wanatarajiwa kuwa tishio katika msimu huu wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
No comments:
Post a Comment