Na Neema Harrison, TUDARCO
KAMATI ya Ardhi, Mawasiliano na Mazingira ya Baraza la
Wawakilishi la Zanzibar, imepongeza kushirikishwa kwa Mamlaka ya Viwanja vya
Ndege Tanzania (TAA), katika mradi wa ujenzi wa Jengo la Tatu la abiria katika
Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bw. Hamza Hassan Juma alitoa
pongezi hizo mara baada ya kutembelea jengo hilo, na kupata maelezo na
ufafanuzi mzuri kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa TAA, Bw.. Salim Msangi, ambayo
yanaonesha kwa kiasi kikubwa wameshirikishwa.
“Hongereni sana kwani huu mradi ni tofauti kabisa tumeona
maelezo yako yanaonesha ni kwa kiasi gani mmeshiriki kuanzia mwanzo wa ujenzi
hadi sasa unakaribia kumalizika, ni tofauti nakwetu siku ya mwisho ndio
tunakabidhiwa mradi na tunakuwa hatujui chochote zaidi ya kukabidhiwa tu,”
amesema Bw. Juma.
Naye Bw. Msangi amesema ndani ya mradi huo kumekuwa na
wahandisi wa idara mbalimbali ikiwemo ya umeme walioanza tangu mradi unaanza
ili baada ya mradi kukamilika inakuwa rahisi na kutambua eneo litakalokuwa na tatizo
kwa ajili ya marekebisho.
Amesema katika ziara hiyo wameweza kujifunza kutoka kwa
Wawakilishi hao ikiwa ni njia ya kupeana uzoefu na chachu ya maendeleo katika
Viwanja Vya Ndege, ambapo katika jengo hilo kuna mifumo ya ukaguzi wa mizigo
hatua tano, na endapo mzigo utakuwa na tatizo unazuiwa kwa ukaguzi zaidi katika
hatua ya mwisho.
“Hii mifumo ni ya kisasa zaidi kwani hata kama abiria akiona
mzigo alioweka na hauruhusiwi kupita kwenye kiwanja chetu, asidhani atakuwa
amesalimika katika hatua ya tano atazuiwa na kufikishwa kwenye vyombo vya
sheria,” amesema Bw. Msangi.
Pia amesema jengo hilo litakuwa mitambo maalum
utakayowatambua kirahisi abiria watakaokuwa wakisafirisha madawa ya kulevyia
wakiwa wameyameza, ambapo awali ilikuwa rahisi kuwatambua kutokana na utaalam
walionao maafisa usalama.
Naibu Waziri wa Ujenzi,Mawasiliano na Usafirishaji wa
Zanzibar, Bw. Mohamed Ahmada Salum amezungumzia kuwa TBIII itatoa ajira kwa
wwatanzania wengi .
Bw. Salum amesema JNIA itarajie mashirika mengi ya ndege
kujitokeza kwa wingi kufanya safari zake, na zitaongeza pato la taifa.
No comments:
Post a Comment