Sunday, 27 August 2017

Simba yaanza kwa kishindo Ligi Kuu Bara

Na Mwandishi Wetu
SIMBA ya Jijini Dar es Salaam imeanza kwa nguvu Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuifunga Ruvu Shooting ya Pwani kwa mabao 7-0 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru.

Mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi (pichani) ameonesha uwezo mkubwa baada ya kufunga mabao manne peke yake katika moja ya mechi saba za ufunguzi wa ligi hiyo.

Mabao mengine ya Wekundu wa Msimbazi, walio chini ya kocha Mcameroon, Joseph Omog anayesaidiwa na Mganda, Jackson Mayanja yamefungwa na Shiza Kichuya, JumaNdanda na Erasto Nyoni.

Okwi alianza kuandika kalamu ya mabao katika dakika ya 18 akimchambua kipa Bidii Hussein baada ya pasi ya Muzamil Yassin na bao la pili akafunga dakika ya 22 baada ya kuwachambua mabeki ndani ya 18 baada ya pasi ya kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Niyonzima.

Okwi akakamilisha mabao matatu au `hat-trick’ ambayo ilimuwezesha kupata mpira wake, alilifunga katika dakika ya 35 baada ya pasi nzuri ya Muzamil tena kabla ya kusaidia kupatikana kwa bao la nne.

Okwi aliwatoka wachezaji wa Ruvu Shoting hadi karibu na boksi na kumpasia beki Erasto Nyoni pembeni kushoto, aliyetia krosi iliyosindikizwa nyavuni na winga machachari, Shiza Kichuya kuipatia Simba bao la nne dakika ya 42.

Mshambuliaji wa zamani wa Zesco United ya Zambia, Ndanda akaifungia Simba bao la tano dakika ya 44 akimalizia krosi ya Nyoni, kabla ya Okwi kufunga bao lake la nne na la sita katika dakika ya 52 kwa kichwa akimalizia krosi ya kiungo Saidi Ndemla.

Beki Erasto Nyoni aliyesajiliwa na Simba akitokea Azam FC alifunga bao la saba katika dakika ya 81 na kuihakikishia timu hiyo ushindi wa mabao 7-0 na kuongoza ligi hiyo.

Katika mechi nyingine za Ligi Kuu siku hiyo ya ufunguzi; Bao pekee la mshambuliaji Mghana, Yahya Mohammed limeipa Azam FC ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Ndanda FC Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

Mwadui imeshinda 2-1 dhidi ya Singida United kwenye Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga, Mtibwa Sugar wameilaza 1-0 Stand United Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro na Mbao FC wameshinda ugenini 1-0 dhidi ya wenyeji, Kagera Sugar Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Tanzania Prisons nayo imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mji Njombe na Mbeya City imeilaza Maji Maji ya Songea 1-0 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.


Ligi hiyo inaendelea tena leo kwa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga watakaposhuka kwenye Uwanja wa Uhuru kucheza dhidi ya timu iliyopanda daraja ya Lipuli ya Iringa.

No comments:

Post a Comment