Thursday, 17 August 2017

JKT yawapongeza wanariadha wake walioshiriki mashindano ya dunia London na kurudi na medali

Wanariadha wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) walioshiriki mashindano ya dunia ya riadha kutoka kushoto ni Alphonce Simbu, Magdalena shauri, Emmanuel Giniki na Stehano Huche wakati wa hafla ya kuwapongeza iliyofanyika Makao Makuu ya JKT Mlalakua leo.
Na Mwandishi Wetu
JESHI la Kujenga Taifa (JKT) limesema kuwa baada ya mwanariadha Alphonce Simbu kurejea na medali kutoka katika mashindano ya 16 ya riadha ya dunia London, Uingereza, wakati umefika kwa wadau kuangalia na michezo mingine ili kulitangaza taifa zaidi.

Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Michael Isamuhyo aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati wa hafla ya kumpongeza mwanariadha Simbu aliyetwaa medali ya shaba katika mashindano hayo ya dunia kwa upande wa marathoni na wenzake.
Mkuu wa JKT, Meja Jenerali, Michael Isamuhyo akipokea saluti kutoka kwa Serviceman, Alphonce Simbu.
Tanzania katika mashindano hayo ilipeleka wanariadha nane, wanne akiwemo Simbu ni waajiriwa wa JKT. Wengine ni Magdalena Shauri, Stephano Huche na Emmanuel Giniki, ambao nao walikuwemo katika hafla hiyo iliyofanyika Makao Makuu ya Jeshi hilo Mlalakua jijini Dar es Salaam.
Isamuhyo alisema kuwa wakati umefika kuangalia na michezo mingine kama ngumi, mpira wa wavu, kuogelea, netiboli na mingine ili nayo iweze kufanya vizuri na kusaidia kuitangaza nchi nje ya mipaka yake.
Hatahivyo, mkuu huyo alisisitiza kuwa Desemba jeshi lake litaongeza wanariadha ili kuhakikisha wanakuwa wengi na kuongeza changamoto katika kambi ya timu hiyo.

Alisema kuwa ana matumaini makubwa kuwa wanariadha hao pamoja na wengine wa Tanzania watafanya vizuri katika mashindano makubwa yajayo.
Aliongeza kuwa wadau wote washirikiane na kuondoa migongano isiyo ya lazima na JKT wako tayari kuwatoa wanariadha hao wakati wowote ili mradi watumike vizuri kwa ajili ya maslahi ya kitaiffa na sio binafsi.
Mkuu wa JKT, Meja Generali, Michael Isamuhyo akisalimiana na mwakilishi wa MultichoiceTanzania, Johnson Mshana huku Katibu Mkuu wa BMT, Mohamed Kiganja akishuhudia leo Mlalakua jijini Dar es Salaam.
Johnson Mshana akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Multichoice-Tanzania, Maharage Chande alisema kuwa watakaa na Simbu ili kujadili mkataba mpya baada ya ule wa awali mwaka mmoja kumalizika baadae mwezi huu.

DStv iliingia mkataba wa mwaka mmoja, ambapo kila mwezi alikuwa akipewa sh milioni 1 kwa ajili ya kujikimu na mkataba mpya unatarajiwa kuwa mnono zaidi ya huo.

Simbu naye aliishukuru JKT, Multichoice-Tanzania, BMT, Riadha Tanzania (RT) kwa mshirikiano na mshikamano waliouonesha hadi kufanikisha ushindi huo wa Tanzania katika mashindanohayo makubwa, ambao alitaka mshikamano huo kuongezeka.
Naye Katibu wa BMT, Mohamed Kiganja alisema kuwa bila majeshi hakuna mafanikio yoyote katika michezo, kwani majeshi yamekuwa na nidhamu kubwa ya kuwalea wachezaji na kuhakikisha wanafanya vizuri.

Katibu Mkuu wa RT, Wilhelm Gidabuday alisema kuwa analishukuru jeshi kwa kuwalea wanariadha hao na kutaka kuwachukua na wanariadha wengine ili kuleta changamoto katika timu yao ya riadha.

 





 









Service Girl, Magdalena Shauri akimrekebisha kofia Serviceman Alphonce Simbu wakati wa hafla ya kuwapongeza wanariadha hao na wenzao walioshiriki mashindano ya dunia ya riadha London, Uingereza.
Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Jenerali Michael Isamuhyo akisalimiana na mwandishi wa The Citizen, Majuto Omary. Katikati ni Katibu Mkuu wa BMT, Mohamed Kiganja.

No comments:

Post a Comment