Na Mwandishi Wetu
KAMATI ya Olimpiki
Tanzania (TOC), imepongezwa kwa kuandaa kwa mara ya kwanza Kozi ya Juu ya
Usimamizi wa Michezo, kwani itakuwa na manufaa katika medani ya michezo.
Pongezi hizo zimetolewa
na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo, Dk Yusuf Singo, wakati
akizindua kozi hiyo kwenye ukumbi wa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.
Singo aliyemwakilisha
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, alisema
mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka kwa sababu hivi sasa michezo inahitaji
kuendeshwa kisasa zaidi.
Alisema kuna vyama ambavyo
alitarajia kuona viongozi wake katika kozi hiyo kutokana na hali ilivyonavyo
lakini hawapo, hivyo TOC iangalie namna ya kuwafikia.
“Michezo inabadilika kila
wakati, viongozi walioongoza zamani ni tofauti na sasa kutokana na mabadiliko.
Ndio maana napenda kusisitiza kuwa elimu hii isambae katika vyama vyote,
ikiwezekana Kamati nzima za Utendaji,” alisema Singo.
Aidha, aliwataka
washiriki wakazanie mafunzo hayo na kuhakikisha wote wanahitimu na kwenda
kuonesha mabadiliko katika utendaji wao na kwamba yeye binafsi atayafuatilia
kwa karibu.
Awali akitoa taarifa fupi
ya kozi hiyo, Mkufunzi Mkuu wa kozi hiyo, Henry Tandau, ambaye atasaidiwa na
Mahmoud Suleiman Jabir, alisema kozi hiyo ni ya kwanza kufanyika hapa nchini.
Tandau, alisema kozi hiyo
itakayokuwa na awamu saba inashirikisha washiriki 15 badala ya 16 kutoka vyama
mbalimbali Tanzania Bara na Zanzibar.
Naye Katibu Mkuu wa TOC,
Filbert Bayi akitoa neno la shukrani, alisema watafanyia kazi suala la kutoa
semina elekezi kwa viongozi wa vyama vya michezo.
Bayi, alisema mara nyingi
wanapoandaa kozi kama hizo, viongozi wakubwa kama Mwenyekiti, Katibu, Muhazina
na wengineo hawajitokeza wakati wao ndio wenye matatizo ya migogoro, badala
yake wanaohudhuria ni viongozi wa kawaida.
Washiriki wa kozi hiyo na
vyama wanavyotokea kwenye mabano ni Nasra Juma Mohamed (Vinyoya Zanzibar), Juma
Zaidi Hamisi (Tenisi Zanzibar), na Musa Abdulrab Fadhil (Mikono Zanzibar).
Wengine ni Amina Ahmed
(Kikapu), Wilfred Kidau, Danny Msangi (TFF), Suleiman Ame Hamis (Riadha
Zanzibar), Sunday Kayuni (Makocha), Asha Muhaji (Taswa), Ruth Kiwia (Mikono),
na Ingridy Kimario (Ofisa Michezo Temeke).
Washiriki wengine ni
Muharami Mchume (Wavu), Juliana Yasoda (Chama cha Michezo cha Wanawake), Irene
Mwasanga (Tenisi), na Mwinga Mwanjala (Riadha).
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini, Dk Yusuf Songo (kushoto) akiteta na Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Gulam Rashid wakati akifungua semina ya juu ya uongozi wa michezo kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam leo.
No comments:
Post a Comment