Thursday, 10 August 2017

Dk. Chamuriho, MAB wakagua ujenzi Kiwanja cha Ndege cha Songwe

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi), Dr. Leonard Chamuriho (wa pili kutoka kulia), Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (MAB), Prof. Ninatubu Lema (wa pili kutoka kushoto), Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Salim Msangi (wa kwanza kushoto) na wajumbe wengine wa MAB wakisikiliza maelezo yanayohusu jengo la abiria la Kiwanja cha ndege cha Kimataifa Songwe kutoka kwa wahandisi, walipotembelea ujenzi huo leo.
Na Mwandishi Wetu
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Serkta ya Uchukuzi), Dk. Leonard Chamuriho leo kwa kushirikiana na Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (MAB), wamefanya ukaguzi wa miundombinu ya barabara ya kutua na kuruka  ndege na jengo la abiria la Kiwanja cha Kimataifa cha Songwe mkoani Mbeya.

Tayari ujenzi wa barabara ya kutua kwa ndege yenye urefu wa km. 3.3 umekamilika, ambapo inaruhusu kutua kwa ndege zenye uwezo wa kubeba abiria kuanzia 90 hadi 300, ambapo ndege za mashirika mbalimbali ikiwemo ya ATCL, Precisions na Fastjet zimekuwa zikifanya safari zake mara kwa mara kwenye kiwanja hicho.
Mhandisi Mshauri wa Kampuni ya Ujenzi ya UNETEC, Roupina Jambazian (aliyenyoosha kidole), akitoa maelezo ya ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege ya Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Songwe. Wa pili kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi), Dr. Leonard Chamuriho na kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Salim Msangi.
Kiwanja hicho kipo daraja la sita (category 6), ambapo mbali na ndege za abiria, pia kinaruhusu kutua kwa ndege za mizigo ya mazao ya kilimo yakiwemo maua, matunda, nyama, mchele na maharage kupelekwa maeneo mbalimbali nchini na nje ya nchi.

Hatahivyo, pia kimekuwa njia kuu inayotumiwa na watalii na wageni wanaotembelea mbuga za wanyama za Ruaha na Kitulo, pia katika vivutio vingine kikiwemo Kimondo kipo Mbozi, Daraja la Mungu lipo Rungwe na Ziwa Ngozi lililopo juu ya mlima baada ya shimo la volkano kujaa maji na kugeuka ziwa.

Ujenzi wa jengo hilo la abiria litakalokuwa na uwezo wa kuhudumia abiria milioni 1.5 kwa mwaka tofauti na jengo la awali linachukua abiria 500,000 pekee, unatarajiwa kumalizika baada ya miezi sita kutoka sasa.
Katibu Mkuu wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya Uchukuzi), Dr. Leonard Chamuriho (aliyechuchuma) akishika upana wa barabara ya kuruka na kutua ndege ya Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Songwe baada ya kupata maelezo kutoka kwa Wahandisi Washauri wa Kampuni ya UNETEC. Mhandisi Roupina Jambazian na Geofrey Asumenye (walioinama), baada ya kufanya ziara pamoja na wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Mamlaka ya Viwanja vya ndege (MAB) ya kukagua maendeleo ya ujenzi  wa miundombinu.

No comments:

Post a Comment