Na Mwandishi Wetu
MSHINDI wa medali ya shaba wa
mashindano ya 16 ya dunia yaliyomalizika jijini London, Uingereza jana, Alphonce
Simbu pamoja na wenzake wanatarajia kuwasili kesho mchana na kupokewa kifalme.
Tanzania katika mashindano hayo
yaliyoanza Agosti 4 na kumalizika jana, ilipeleka wanariadha wanane lakini
Simbu peke yake ndiye aliyetwaa medali katika mbio za marathoni kwa kutumia saa mbili na dakika tisa katika nafasi ya tatu.
Hiyo ni medali ya kwanza kwa Tanzania
kupata baada ya miaka 12 baada ya Christopher Isegwe kumaliza wa pili na kupata
medali ya fedha katika mbio za marathoni na kuondoka na medali ya fedha katika
mashindano yaliyofanyika Helsinki, Finland mwaka 2005.
Katibu Mkuu wa Riadha Tanzania (RT),
Wihlehm Gidabuday amesema leo Jumatatu kuwa Simbu na wenzake wataata mapokezi
makubwa watakaowasili kwenye Kiwanja cha Kimataifa cha Ndege cha Julius Nyerere
(JNIA) kesho mchana kwa ndege ya Emirates wakitokea London kupitia Dubai.
Mara baada ya kuwasili, timu hiyo
itapokewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Harrison Mwakyembe
na kufanya mkutani na waandishi wa habari katika kiwanja hicho kuelezea
yaliyojiri London.
Kwa mujibu wa Gidabuday, nje ya kiwanja
hicho kunatarajia kuwepo burudani kadhaa vikiemo vikundi vya JKT
vitakavyoburudisha wanariadha hao pamoja na wadau mbalimbali wa michezo na hasa
riadha watakaofika kuwaokea akina Simbu.
Inaelezwa kjuwa Simbu anayedhaminiwa na
DStv na wachezaji wengine watakuwa ndani ya gari la wazi, ambalo litawazungusha
katika kitaa mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam wakipitia Ilala, Kariakoo na
kwingineko kabla ya kutua katika hoteli ya Protea iliyopo Oysterbay jirani na
kanisa la Mtakatifu Petro (St Peter’s), ambako Simbu atapumzika kabla ya keshokutwa kwenda kwao Arusha.
Mbali na Simbu, wanariadha wengine
waliokuwemo katika timu hiyo ni pamoja na Stephano Huche, Ezekiel Ngimba, Sarah
Ramadhani na Magdalena Shauri (Marathoni), Failuna Abdi (Meta 10,000), Gabriel
Geay na Emmanuel Giniki (Meta 5,000).
Geay hakukimbia katika mbio zake
kutokana na kuwa majeruhi huku Shauri akishindwa kumaliza baada ya kukimbia kwa
zaidi ya kilometa 25 kutokana na kuwa na maumivu aliyokuwa nayo hata kabla ya
kuondoka nchini.
Nyota ya Simbu ilianza kung’ara katika
Michezo ya Olimpiki iliyofanyika Rio, Brazil 2016 wakati alipomaliza wa tano kwa
kutumia saa 2;11:15 kabla ya kumaliza wa kwanza katika Mumbai Marathoni
mwanzoni mwa mwaka huu alipotumia saa 2:09:32, kabla ya kuboresha zaidi muda wake bora binafsi pale aliomaliza wa tano
kwa kutumia saa 2:09:10 katika London Marathoni licha ya kuibuka watano.
No comments:
Post a Comment