ALGIERS, Algeria
TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Congo imejiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa taji la Shirikisho la Afrika
baada ya kutoka sare dhidi ya Mouloundia Olympique de Bejaia katika mchezo wa
kwanza wa fainali uliofanyika mjini hapa.
Mabingwa hao wazamani wa Ligi ya Mabingwa wa
Afrika wamejiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa huo wa Shirikisho
kufuatia sare hiyo katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Stade Mustapha
Tchaker El Bouleïda mjini Blida
juzi usiku.
Mabao hayo yalifungwa katika kila kipindi
kupitia kwa Jonathan Bolingi na Faouzi Yaya yaliviwezesha vigogo hivyo kila
mmoja kuondoka na pointi moja.
Kwa sare hiyo, TP Mazembe inahitaji suluhu au
ushindi wa aina yoyote ili kutangaza ubingwa wa mashindano hayo ya Afrika.
Yacine Athmani nusura afunge bao mwanzoni mwa
mchezo huo baada ya kupiga shuti la mbali, lakini lilikwenda moja kwa moja
mikononi mwa kipa Sylvain Gbohouo katika dakika tatu tangu kuanza kwa mchezo
huo.
Ingawa timu zote zilijaribu kuzifumania nyavu
ndani ya dakika 30, lakini walikuwa wageni Mazembe ndio waliweka presha kwa
wenyeji wao Mo Bejaia.
Zikiwa zimebaki dakika mbili kabla ya mchezo
kuwa mapumziko, wageni walifanikiwa kufunga bao lao la kwanza kupitia kwa Bolingi
kwa penalti. Hadi kipindi cha kwanza kinamalizka, ubao ulionesha 1-0 kikosi cha
Hubert Velud kikiongoza.
Hatahivyo, baada ya kurejea uwanjani, nahodha
wa Bejaia, Yaya aliwafungia bao wenyeji la kusawazisha katika dakika ya 66.
Mchezo wa Marudiano umepangwa kupigwa
Jumapili Novemba 6 kwenye Uwanja wa Stade du TP Mazembe jijini Lubumbashi ili
kumpata bingwa.
Mazembe iliwahi kuifunga Bejaia mara moja
nyumbani mwaka huu, 1-0 katika hatua ya makundi, huku mchezo uliopita
uliofanyika Algeria ulimalika kwa suluhu.
Mazembe imeshinda mara tisa taji la Ligi ya
Mabingwa wa Afrika lakini haijawahi kushinda taji la Shirikisho, ambapo mshindi
ataondokana kitita cha dola za Marekani 660,000 (sawa na sh bil 1.4) huku
mshindi wa pili ataondoka na dola 462,000 (sh bil 1).
Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ambao ni
mabingwa wapya wa Ligi ya Mabingwa wa Afrika wenyewe mbali na fedha taslimu pia
watawakilisha bara la Afrika katika mashindano ya Klabu Bingwa ya Dunia.
No comments:
Post a Comment