Monday, 24 October 2016

Riadha Tanzania kuchaguana Novemba 27 Dar es Salaam fomu za kuwania uongozi kuanza kutolewa Novemba mosi


Kaimu Katibu Mkuu wa Riadha Tanzania (RT), Ombeni Zavalla.


Na Mwandishi Wetu
UCHAGUZI Mkuu wa Riadha Tanzania (RT) utafanyika Novemba 27 jijini Dar es Salaam, imeelezwa.

Hatua hiyo ya kupanga tarehe na mahali pa kufanyikia uchaguzi huo ilifikia mwishoni mwa wiki iliyopita katika kikao cha Kamati ya Utendaji kilichofanyika katika ukumbi wa Filbert Bayi Sports Complex Mkuza, Kibaha.

Kaimu katibu mkuu wa RT, Ombeni Zavalla alisema kuwa hutoaji fomu utaanza Novemba mosi katika ofisi za RT zilizopo katika ofisi za zamani za Baraza la Michezo la Taifa (BMT).

Alisema nafasi zitakazogombewa ni ya Rais, Makamu wawili wa rais (utawala na fedha na yule atakayehusika na ufundi), katibu mkuu, katibu mkuu msaidizi, mhazini na wajumbe wa Kamati ya Utendaji.

Alisema wale watakaochukua fomu za kutaka urais, makamu, katibu, katibu msaidizi na mhazini, kila mmoja atanunua fomu kwa sh. 150,000 wakati wajumbe fomu zao zitapatikana kwa sh. 100,000 kila moja.

Zavalla alisema kuwa wameamua kurudisha nyuma uchaguzi wao badala ya Desemba ili kupisha Uchaguzi Mkuu wa TOC utakaofanyika Desemba 10 mjini Dodoma.

Alisema kila mkoa utakuwa na wajumbe watatu watakaoingia katika mkutano mkuu huo wa uchaguzi baada ya msajili kukataa marekebisho ya kipengele kilichotaka kila mkoa kuwa na mjumbe mmoja tu.

Alisema uchaguzi huo utatanguliwa na mkutano mkuu,ambao utajadili masuala mbalimbali ikiwemo ripoti ya mwaka, taarifa ya fedha na mambo mengine.

Aidha, Zavalla alisema kuwa kikao hicho cha Kamati ya Utendaji kilipitia pia taarifa za mashindano mbalimbali yakiwemo yale ya Olimpiki ya Rio 2016, ambayo mwanariadha Alphonce Simbu alimaliza wa tano.

No comments:

Post a Comment