Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imezipiga stop Yanga na Simba kuendelea na michakato yao
ya kubadili umiliki wa klabu hizo hadi pale yatakapofanyika marekebisho ya
katiba zao.
Hayo yalitangazwa leo na Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo
la Taifa (BMT), Mohamed kiganja wakati akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam.
Kiganja alisema kuwa Serikali haikatai mabadiliko ya uendeshaji
katika klabu hizo pamoja na zingine za wanachama, ila inachotaka kwanza
kufanyike marekebisho ya katiba zao, ambayo sasa hayaruhusu mabadiliko hayo.
Alisema kuwa BMT inapenda kuona kwamba wahusika wanafuata sheria
na taratibu za nchi katika kufikia malengo yao, ambapo alisisitiza kuwa
kuendelea na michakato hiyo kabla ya kurekebisha katiba zao ni kosa na hatua
kali zitachukuliwa dhidi yao.
“Hivi karubuni kumeibuka
michakato ya watu wakitaka kubadilisha umiliki wa klabu za wanachama na
kuzielekeza katika utaratibu wa hisa na ukodishwaji, vitendo vimesababisha
migogoro mikubwa ambayo inaashiria uvunjifu wa amani…”
Kiganja alisema tayari mezani kwake kuna barua kibao za wanachama
wa Yanga wanaopinga vikali kuendelea kwa mchakato huo wa kubadilisha umiliki.
Ibara ya 56 ya Katiba ya Yanga iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010
inaeleza kuhusu kampuni ya umma:
Inaeleza kuwa kutakuwa na kampuni itakayojulikana kama Young
African Sports Corporation Limited ambayo itasajiliwa chini ya sheria ya
makampuni kama kampuni ya umma yenye hisa.
Sehemu ya pili ya ibara hiyo inasema wanachama wote katika klabu
ambao katika tarehe ya marekebisho ya Katiba ya mwaka 2007 wako hai
watakuwa,kwa nguvu ya uanachama wao, wanahisa katika kampuni kwa kiwango cha
idadi ya hisa watakapopata kwa mujibu wa muafaka wa Yanga uliofikiwa na Wana
Yanga Juni 22, 2006.
Klabu itamiliki hisa zilizosawa na asilimia 51 ya hisa zote
zilizomo katika klabu hiyo.
Mkutano Mkuu wa Uchaguzi utachagua wanachama wawili, ambao sio
miongoni mwa viongozi wa klabu kuwa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa kampuni
kwa ajili ya kuwakilisha maslahi ya klabu kwenye kampuni.
Tayari Yanga iko chini ya Kampuni ya Yanga Yetu ambayo ni mali ya
mwenyekiti wa klabu hiyo Yusuf Manji, ikiwa ni kinyume na katiba yao wenyewe.
Kiganja alisisitiza kuwa klabu zisitishe mipango ya kubadilisha
uendeshaji na ziendelee kuwa mali ya wanachama.
Wakati Yanga walikuwa tayari wameishaingia mkataba wa miaka 10 wa
kuikodisha klabu yao, wenzao wa Simba walijipa miezi sita kukamilisha taratibu
za kuuza hiza.
No comments:
Post a Comment