Monday, 24 October 2016

Real Madrid yaishusha Sevilla kileleni baada ya kuifunga Athletic Bilbao katika La Liga



MADRID, Hispania
REAL Madrid imeishusha kileleni Sevilla na kushika uongozi huo wa La Liga baada ya kupambana kiume na kuifunga Athletic Bilbao.

Awali, Sevilla ilishika kwa muda uongozi wa ligi hiyo baada ya kuifunga Atletico Madrid kwa bao 1-0 katika mchezo uliofanyika mapema Jumapili.

Karim Benzema aliiweka Real Madrid mbele kwa 1-0 baada ya kufunga bao kufuatia pasi ya Isco.

Lakini Sabin Merino alisawazisha baada ya Pepe na Dani Carvajal kushindwa kuchukua mpira kutoka kwa Javier Eraso.

Cristiano Ronaldo aliwakosesha wenyeji nafasi kibao za kuifungia mabao Real lakini Alvaro Morata aliyeingia akitokea benchi katika siku yake ya kuzaliwa akitimiza miaka 24, ndiye alikuwa shujaa wakati akifunga bao katika jaribio lake la pili baada ya Gorka Iraizoz kuokoa shuti lake.

Real Madrid ni timu ya nne wikiendi hii kushika usukani wa La Liga. Barcelona ilishika usukani Jumamosi shukrani kwa bao la ushindi la dakika za mwisho lililoifanya timu hiyo kutoka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Valencia.

Mapema Jumapili, Sevilla ilishika uongozi wa ligi hiyo baada ya kuifunga Atletico Madrid kwa bao 1-0.

Pointi tatu tu ndio zilikuwa zikizitofautisha Real, ambayo iliuanza mchezo wa Jumapili ikiwa katika nafasi ya tano kabla ya kushika usukani baada ya ushindi wake huo.

No comments:

Post a Comment