BRASILIA, Brazil
BRAZIL imetinga kileleni mwa
msimamo wa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2018 kwa Kanda ya Amerika ya
Kusini, baada ya kuibuka na ushindi dhidi ya Venezuela wakati Argentina ikipokea
kichapo nyumbani kutoka kwa Paraguay.
Mabao kutoka kwa chipukizi
wa Manchester City, Gabriel Jesus na mchezaji wa Chelsea Willian yaliiwezesha
timu hiyo kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Venezuela katika mchezo
ulioingiliwa na kuzimika kwa taa na kuufanya Uwanja wa Metropolitano wa Estadio
kuwa giza.
Ushindi huo ni wa nne
mfululizo kwa Brazil katika kampeni hizo za kufuzu na kuwaacha mabingwa hao
mara tano wa dunia kuongoza katika msimamo wakiwa na pointi 21 baada ya kushuka
dimbani mara 10.
Ushindi huo pia ni ushahidi
wa hivi karibuni kabisa kuwa Brazil chini ya kocha mpya Tite, aliyeichukua timu
hiyo baada ya kutimuliwa kwa Dunga Juni baada ya timu hiyo kufanya vibaya katika
michuano ya Copa America Centenario, iko vizuri.
Ni mara ya kwanza kwa Brazil
kuongoza msimamo huo tangu kuanza kwa kamapeni za kufuzu, na timu inaonekana
ikiendelea vizuri na inaelekea kuendeleza rekodi yake ya kutowahi kushindwa
kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia.
Hatahivyo, mtihani mkubwa
kwa Brazil utakuwa mwezi ujao na hapo ndipo itadhihirisha kama makali yao sio
ya muda wakati itakapokutana na wapinzani wao wazamani Argentina, ambao juzi
walipokea kichapo cha bao 1-0 nyumbani kutoka kwa Paraguay huko Cordoba.
Bao lililotokana na
shambulizi zuri la kushtukiza kutoka kwa mshambuliaji Derlis Gonzalez katika
dakika ya 18 lilitosha kabisa kuipatia Paraguay pointi zote tatu wakati wenyeji
kwa mara nyingine tena wakijaribu kuzoea kucheza bila nyota wao wanaomtegemea
sana Lionel Messi.
Argentina imeambulia pointi
mbili tu badala ya tisa zilizotakiwa katika mechi zake tatu zilizopita, ambazo
zote walikipiga bila yakuwepo Messi.
Timu hiyo ya Argentina
ilionekana kubadilika katika kipindi cha pili, huku Angel Di Maria akinusurika
kufunga baada ya mpira wake wa adhabu kushindwa kutinga wavuni huku Gonzalo
Higuain na Sergio Aguero nao wakikaribia kupata mabao.
Ushindi huo umeiacha Paraguay
ikiwa pointi moja nyuma ya Argentina katika msimamo baada ya mechi 10. Argentina
iko katika nafasi ya tano kimsimamo ikiwa na pointi 16, huku Paraguay ikiwa
nyumabaada ya kujikusanyia pointi 15.
Wakati huohuo, Chile, imeendelea kuwa nje ya nafasi ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2018 licha ya juzi kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Peru katika mchezo uliofanyika Santiago katika mchezo ambao wengi wanautambua kama "Clasico del Pacifico."
Chile,ambayo katika miaka
miwili iliyopita ilitawala soka la Amerika ya Kusini kwa kushinda mara mbili
mfululizo taji la Copa America, ilihitaji pointi tatu ili kurejea katika mstari
baada ya kuanza vibaya kampeni zake hizo za kufuzu.
Kiungo wa Bayern Munich
Atrudo Vidal aliipatia bao "La Roja" au `Wekundu’ kama
inavyojulikana timu ya taifa ya Chile, na kuipatia matumaini ya kufanya vizuri
kwa bao hilo la kuongoza la dakika ya 10 na kuifanya Chile kuwa mbele kwa bao
1-0.
Juhudi za Peru zilizaa
matunda katika dakika ya 76 wakati Edison Flores alipofunga bao kwa shuti
hafifi na kufanya matokeo kuwa 1-1.
Ilionekana kama Peru
imefanikiwa kuondoka na pointi moja wakati muda ukuzidi kuyoyoma, lakini Vidal alipata
nafasi katika eneo la penalti na kupiga shuti hafifu lililompita Pedro Gallese
na kujaa wavuni.
Ushindi huo wa Chile
umeiacha timu hiyo ikiwa ya saba katika msimamo kwa kuwa na pointi 14, mbili
kutoka nafasi za kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia.
Mapema, vinara Uruguay walitoka
sare ya mabao 2-2 na timu ya Colombia iliyopo katika nafasi ya nne.
No comments:
Post a Comment