Na Mwandishi Wetu
GABRIEL Gerald amevunja rekodi ya Dar Rotary
Marathon wakati wanariadha wengine wa Tanzania wakitamba katika mbio hizo
zilizofanyika jana na kuhudhuriwa na maelfu.
Mwanariadha huyo alimaliza mbio hizo kwa
kutumia saa 1:01:49 wakati rekodi iliyopo ni ya saa 1:02, huku akiwapita
wanariadha walioshiriki Michezo ya Olimpiki ya Rio 2016 nchini Brazil.
Wanariadha wa Tanzania, Felix Alphonce (kulia) na Dickson Marwa wakiteta kabla ya kuanza kwa mbio za kilometa 21 za Dar Rotary Marathon leo.
|
Alphonce Felix na Fabian Joseph walioshiriki
Michezo ya Olimpiki 2016 walijikuta wakipigwa bao na Gerald ambaye alikosa
sekunde nne tu kufuzu kwa Olimpiki katika mbio za meta 10,000, walipomaliza
katika nafasi ya tatu na 12.
Mwanariadha mwingine wa Tanzania kwa upande
wanaume walioshiriki Olimpiki, Said Makuka alikuwepo jana, lakini hakushiriki
mbio hizo. Mshindi wa pili alikuwa Ismail Juma aliyetumia saa 1:01:52 huku
Benard Msau na Peter Kipte wote wa Kenya wakimaliza wa nne na tano kwa kutumia
saa 1:02:25 na 1:03:14.
Kwa upande wa wanawake, Mnyarwanda Salome
Nyirarukundo alifanikiwa kutetea ubingwa wake wa mwaka jana baada ya jana
kumaliza wa kwanza kwa kutumia saa 1:11.34.68 huku Mtanzania Failuna Abdi
akimaliza wa pili kwa saa 1:12:27 na Angela Daniel alimaliza wa tatu kwa saa
1:13:22:23 na Sara Ramadhani alimaliza wa nne kwa saa 1:14:34.23.
Nyirarukundo ndiye mwanariadha bora wa Rwanda
wa mwaka 2016 baada ya kuwapiku wenzake kwa mbali katika kura za uteuzi.
Alphonce, ambaye ni mshindi wa tano wa
Olimpiki ya Rio katika marathon, alisema mbio zilikuwa ngumu hasa ukizingatia
kuwa ndio kwanza ameanza mazoezi baada ya kuwa katika mapumziko kutokana na
Michezo ya Olimpiki.
Alisema siku zote mshindi ni yule
aliyejiandaa vizuri na alimpongeza Gerald kwa ushindi huo na alisema ndio
ameanza mazoezi kwa mashindano mbalimbali.
Mshindi wa mbio hizo, Gerald alisema mbio
zilikuwa nzuri na zenye ushindani wa hali ya juu na alishinda kwa sababu
alijiandaa vizuri.
Nyirarukundo alisema mbio zilikuwa nzuri na
alishinda kwani ndio kwanza alirejea kutoka katika Michezo ya Olimpiki ya Rio
2016, ambako alishiriki mbio za meta 10,000.
Mbio hizo ziliongozwa na rais mstaafu wa
awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi ambaye alishiriki matembezi ya kilometa tano
na baadaye alitoa zawadi kwa washindi.
Mwinyi alisema kuwa mbio hizo zinazidi kukua
na kuwapongeza waandaaji kufanikisha mbio hizo za tisa tangu kuanza kwake.
No comments:
Post a Comment