Neymar wa Brazil (kulia) akichuana na mchezaji wa Bolivia, Yasmani Duk wakati
wa mchezo wa kufuzu kwa Kombe la Dunia Urusi 2018 uliofanyika jana Natal,
Brazil. Wenyeji walishinda mabao 5-0.
|
BRASILIA, Brazil
MCHEZAJI nyota Neymar alifunga bao moja na
kutengeneza mengine mawili zaidi wakati Brazil ikiibuka na ushindi mnono wa
mabao 5-0 dhidi ya Bolivia katika mbio za Amerika ya Kusini za kufuzu kwa
fainali za Kombe la Dunia 2018.
Neymar, ambaye ni nyota wa Barcelona alifunga bao la 49 katika mechi ya
kimataifa ikiwa ni mara yake ya 73 kuichezea Brazil na kumzidi Zico katika
ufungaji wa mabao mengi wa wakati wote.
Akiwa bado na umri wa miaka 24 tu, Neymar
anaweza kufikia rekodi ya Pele ya kufunga mabao 77 kutoka katika mechi 91 huku
akiwa bado namechi kadhaa kabla ya kufikia 91.
Ushindi huo wa Brazil umeiacha timu hiyo
ikiwa katika nafasi nzuri ya kutwaa nafasi ya kufuzu kwa fainali ya Kombe la
Dunia 2018 nchini Urusi.
Timu hiyo sasa inashika nafasi ya pili katika
msimamo ikiwa na pointi 18 baada ya kucheza mechi tisa.
Pia huo ni ushindi wa tatu mfululizo kutoka
katika mechi tatu kwa kocha Tite, aliyeteuliwa baada ya kutimuliwa kwa Dunga
Juni.
Mbali na Neymar, wachezaji wengine walioing’arisha Brazil kwa mabao ni
pamoja na Philippe Coutinho, Filipe Luis na
Gabriel Jesus na kuiwezesha timu hiyo kuwa mbele kwa mabao 4-0 hadi
kipindi cha kwanza kinamalizika.
Mchezaji mwenzake Coutinho katika Liverpool,
Roberto Firmino alifanya matokeo kuwa mbele kwa 5-0 kwa bao la kichwa
lililofungwa katika dakika ya 75.
Neymar aliifungia Brazil bao la kuongoza
katika dakika ya 10 tu. Brazil sasa
itasafiri hadi Venezuela kucheza Jumanne dhidi ya timu hiyo ambayo haijashinda
hata mchezo mmoja.
No comments:
Post a Comment