Na Mwandishi Wetu
MWILI wa bondia wa ndondi za kulipwa nchini, Thomas
Mashali aliyeuawa Kimara jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia Jumatatu,
utazikwa leo kwenye makaburi ya Kinondoni.
Baba mzazi wa marehemu, Malifedha Mashali alisema kuwa
mwili wa mtoto wake huyo aliyeuawa kwa kupigwa na watu wasiojulikana, utazikwa
katika makaburi ya Kinondoni Mwembejini.
Alisema mipango mingine ya mahali utakapoagiwa mwili
huo na utakapoombewa, bado ilikuwa inaendelea na alikuwa hajajua shughuli hizo
zitafanyikia wapi.
Mzee Mashali alisema kuwa mwili wa mtoto wake utaagwa
katika viwanja vya Leaders Club Kinondoni kuanzia saa 7 mchana kabla ya
kwenda kupumzishwa katika nyumba yake ya mileleni katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Mashali alikuwa akishikilia mikanda ya WBO na UBO
kabla ya kifo chake, ambapo amekufa huku akiacha mataji kibao ya ngumi ya hapa
nchini na yale ya kimataifa.
Wadau wengi wa michezo walitoa masikitiko yao kuhusu
kifo hicho cha Mashali huku wengi wao wakisema kuwa bondia huyo alikuwa na
kipaji cha aina yake katika ndondi.
Mashali alizaliwa Dar es Salaam mwaka 1989 na alianza
kupigana ngumi za kulipwa Novemba 27, 2009 alipopigana na kumtwanga Hamadu
Mwalimu katika pambano lililofanyika katika ukumbi wa Texas, Manzese.
No comments:
Post a Comment