Na Mwandishi Wetu
SIMBA leo imeonja chungu ya kufungwa baada ya kupokea kichapo cha mabao 2-1 na Coastal Union ya Tanga katika mchezo wa Kombe la FA katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kwa matokeo hayo, Simba imetupwa nje ya mbio za kusaka nafasi ya kuliwakilisha taifa katika mashindano ya Kombe la Shirikisho la Afrika. Bingwa wa FA hushiriki Kombe la Shirikisho la Afrika mwakani.
Coastal Union wako katika hatari ya kushuka daraja
katika Ligi Kuu Tanzania Bara kufuatia kushika mkia katika msimamo wa ligi hiyo
ikiwa na pointi 19 baada ya kucheza mechi 26 wakati Simba wanaoongoza kwa kuwa
na pointi 57 baada ya kushuka dimbani mara 24.
Katika mchezo huo, Coastal Union ndio walikuwa wa
kwanza kupata bao katika dakika la 19 lililofungwa na Yusuph Sabo baada ya
kupiga mpira wa faulo uliokwenda moja kwa moja wavuni.
Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, Coastal Union walikuwa
mbele kwa bao hilo moja licha ya Simba kutawala zaidi kipindi hicho.
Kipindi cha pili kilipoanza Simba ilifanya
mabadiliko, ambapo iliwatoa Said Ndemla na Justice Majbvi na kuwaingiza Hamisi
Kiiza na Awadhi Juma.
Kiiza aliisawazishia Simba baada ya kuunganisha kwa
kichwa krosi ya Ibrahim Ajibu katika dakika ya 51.
Dakika ya 83 Yusuph Sobo aliifungia Coastal Union
bao la pili kwa penalti baada ya Novaty Lufunga kumchezea vibaya Ahmed Shiboli
ndani ya eneo la hatari. Lufunga alitolewa nje kwa kadi nyekundu kutokana na
rafu hiyo.
Naye Grace Mkonjera anaripoti kuwa, ratiba ya nusu
fainali ya Kombe la Shirikisho la TFF, inatarajiwa kufanyika leo usiku kuanzia
saa 3 usiku na kurushwa moja kwa
moja kupitia kituo cha luninga cha AzamTwo.
Coastal inaungana na timu za Azam FC, Mwadui FC, na
Yanga SC zilizotangulia kucheza nusu fainali ya mashindano hayo.
Katika mechi za Ligi Kuu Simba imeifunga Coastal
mara mbili, ambapo mara ya kwanza ilishinda 1-0 Oktoba 28, 2015 kwenye Uwanja
wa Taifa kabla ya kuichapa tena 2-0 Machi 19 mwaka huu kwenye Uwanja wa
Mkwakwani mjini Tanga.
Sasa Simba ambayo haijashiriki michuano ya kimataifa
kwa miaka kadhaa, huenda mwakani ikaendelea kukaa kando baada ya kubaki na
nafasi moja tu ya kucheza Ligi ya Mabingwa wa Afrika, endapo itatwaa ubingwa wa
Tanzania Bara.
No comments:
Post a Comment