Na Mwandishi Wetu
RATIBA ya Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports
Federation Cup) imefanyika usiku wa jana, huku timu za Coastal Union na Mwadui FC zikipata nafasi ya
kucheza nyumbani.
Katika droo hiyo iliyochezeshwa na mchezaji mstaafu wa timu ya taifa ya wanawake (Twiga Stars), Esther Chaburuma, vigogo
wa Ligi Kuu ya Vodacom, Azam FC na Yanga wakipata nafasi ya kucheza
michezo hiyo katika viwanja vya ugenini.
Mwadui FC watakua wenyeji wa Azam FC katika mchezo unaotarajiwa
kucheza Aprili 24, 2016 mjini Shinyanga, huku Wagosi wa Kaya Coastal Union
wakicheza dhidi ya Yanga katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga siku
hiyo hiyo.
Washindi wa michezo hiyo ya Nusu Fainali, watakutana fainali ya
kombe hilo itakayofanyika mwezi Mei, ambapo Bingwa wake ataiwakilisha Tanzania
katika michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF CC).
Wakati huohuo, wadhamini wa michuano hiyo Azamtv kupitia kituo
chake cha michezo cha Azam Sports, walilionesha hadharani kwa mara
ya kwanza kombe la ubingwa na kulikabidhi kwa Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa
Selestine.
No comments:
Post a Comment