Wanafunzi wavulana wa shule za sekondari wakianza mbio za kilomita 2.5 za Ngorongoro Marathon mjini Karatu leo. |
Na Mwandishi Wetu, Karatu
MBIO za tisa za Ngorongoro Marathon zimefanyika jana huku
mwanariadha wa taifa Ismail Juma akivunja rekodi ya mbio hizo kwa kutumia saa 1:02.48
na kuipiku ile ya awali ya saa 1:03.00 iliyowekwa miaka mingi iliyopita.
Juma tangu mwanzo wa mbio hizo alionesha kila dalili ya kuibuka na
ushindi tena mnono baada ya kuwaacha wenzake kwa mbali na kumaliza wa kwanza na
kushinda mshindi wa pili kwa dakika nne zaidi, kitu ambacho ni nadra sana
kutokea katika mbio zozote.
Wanafunzi wakichuana katika mbio za kilometa 2.5 za Ngorongoro Marathon mjini Karatu leo. |
Mbio hizo zilianzishwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa
Jumanne Maghembe ambaye baadae alishuhudia Juma akivunja rekodi ya mbio hizo
zilizoanzia katika lango la kuingilia na kutokea katika Hifadhi ya Ngorongoro
na kumalizikia kwenye viwanja vya Mazingira Bora mjini Karatu.
Baada ya kukimbia katika kundi moja na wenzake kwa karibu kilomita
nne, Juma aliwaacha kuanzia hapo hadi mwisho wa mbio huku wenzake wakibaki
wakisoma namba.
Washiriki wa mbio za kilometa 21 za Ngorongoro Marathoni wakijiandaa kwa mbio hizo leo katika lango la kuingilia na kutokea Hifadhi ya Ngorongoro. |
Juma alimzidi mshindi wa pili kwa takribani dakika nne baada ya
Stephen Uche kumaliza mbio hizo kwenye Uwanja wa Mazingira Bora mjini Karatu
akitumia saa 1:06.3 huku Yohana Elisante akishika nafasi ya tatu kwa saa
1:06.24.
Mwanariadha huyo ni miongoni mwa wanariadha wanaounda timu ya taifa
inayotarajia kushiriki Michezo ya 31 ya Olimpiki itakayofanyika baadae mwaka
huu Rio, Brazil na atakimbia mbio za mita 5,000 na 10,000 endapo atafuzu.
Kwa upande wa wanawake, Fainuna Abdi ameendelea kuwaburuza
wakongwe baada ya kuibuka wa kwanza katika mbio hizo kwa kutumia saa 1:11.52 na
kumzidi mchezaji wa timu ya taifa Nathalia Elisante aliyemaliza wa pili kwa
kutumia saa 1:15.46 huku Fadhila Tipa akiwa wa tatu kwa saa 1:16.54.
Kocha wa timu ya taifa ya Ridha inayojiandaa kwa Michezo ya
Olimpiki iliyopiga kambi West Kilimanjaro mkoani Kilimanjaro, Francis John akizungumza
kwa njia ya simu jana alisema Juma alistahili kushinda kwani yuko vizuri
kutokana na mazoezi aliyofanya.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe (wa pili kulia) akianzisha mbio za tisa za Ngorongoro leo. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Omary Qwang na kushoto ni Mama Zara. |
Alisema hata kabla ya mbio alimuahidi kocha wake kuwakimbiza
wenzake hadi watu washangae, na ni kitu ambacho amekifanya jana kwa kuwaacha
wenzake mbali.
Naye Juma akizungumza baada ya kumaliza mbio hizo alisema siri ya
mafaniki yake ni mazoezi ya muda mrefu anayoendelea kufanya katika kambi ya
timu ya taifa.
Naye Maghembe alisema anataka mbio za 10 za Ngorongoro ziwe za
kimataifa zaidi kwa kutoa wanariadha watakashiriki na kushinda katika marathoni
za kimataifa kama zile za London, New York, Boston na zingine.
Kwa miaka mingi sasa wanariadha wa Tanzania wameshindwa kabisa
kushiriki katika mbio kubwa za kimatiafa kutokana na kuwa na viwango vidogo,
ambavyo haviwawezeshe kushiriki tofauti na miaka ya nyuma.
Wanariadha kama akina Juma Ikangaa, Francis Nade, Zebedayo Bayo,
Simon Mrashani, Lwiza John, Francis Naali na wengine wengi walishiriki mbio
mbalimbali kubwa za mialiko kutokana na kuwa na muda mzuri kimataifa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Omary Qwaang alisema kuwa vijana
waendelee kujiweka fiti ili waweze kufanya vizuri katika mbio hizo na zingine
na kulipatia sifa taifa.
Alisema kuwa mashindano ya Ngorongoro yanawapa matumaini makubwa
ya wanariadha wetu kufanya vizuri katika mashindano yajayo ya kimataifa.
Mbio hizo za tisa za Ngorongoro zimefanyika huku huku kukiwa na
mvua kubwa iliyoanza kunyesha tangu juzi na kuendelea siku nzima ya jana.
Mbali na mbio za kilomita 21 kwa wanawake na wanaume, pia
kulikuwepo mbio za kilometa tano kwa ajili ya makampuni na taasisi mbalimbali
pamoja na zile za kilomita 2.5, ambazo ziliwashirikisha wanafunzi wa shule za
msingi na sekondari.
Mbio za mwaka huu zimedhaminiwa na Zara Charity pamoja na Zara
Tours, Bonite Bottlers, Malenga Investment, Exim Bank, Equity Insurance, Davis
Mosha na African Safari.
No comments:
Post a Comment