Wednesday, 6 April 2016

Wanariadha wazidi kujitokeza kujiandikiza kushiriki Ngorongoro Marathon 2016, Mkuu wa mkoa wa Arusha athibitisha kushiriki mbio hizo



Baadhi ya wanariadha wakichuana katika mbio za Ngorongoro zilizofanyika mwaka jana.

Na Mwandishi Wetu
WANARIADHA kibao wamezidi kujitokeza kujiandikisha kwa ajili ya kushiriki mbio za Ngorongoro zitakazofanyika Aprili 16 mwaka huu, imeelezwa.

Mbio za mwaka huu zinatarajia kuwa na msisimko wa aina yake huku tayari wanariadha zaidi ya 700 kutoka ndani na nje ya nchi wakiwa wamejiandikisha kwa ajili ya mbio hizo.

Mratibu wa Ngorongoro Marathon 2016, Zulfa Fadhili alisema jana kuwa, usajili wa wanariadha wanaotaka kujiandikisha unaendelea katika vituo kadhaa pamoja na katika mtandao.

Fadhili alivitaja baadhi ya vituo hivyo kuwa ni pamoja na Arusha katika duka la Lemaya, wakati Karatu Deus Super Market huku Moshi usajili unafanyika katika ofisi za Zara na Malenga Investment.

Aliwataka wanariadha kuendelea kujiandikisha kwa ajili ya ushiriki wa mbio hizo, ambazo mwaka huu zinatarajia kuwa na msisimko wa aina yake.

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Daud Ntibenda, ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha akizungumza wakati wa mbio za mwaka juzi katika Uwanja wa Mazingira Bora mjini Karatu.
Aidha, Fadhili alisema kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Daud Ntibenda amethibitisha kushiriki mbio hizo ambazo mgeni rasmi anatarajia kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Jumanne Maghembe.

Lengo la mbio hizo ambazo zinadhaminiwa na Bonite Bottlers, Zara Charity na Zara Tours, Davis Mosha, Malenga Invstment, Exim Bank na African Safaris, ni kuchangisha fedha kwa ajili ya kuendesha shule za watoto wa Kimaasai, ambao wanasomeshwa bure.

No comments:

Post a Comment