Na Mwandishi Wetu
NCHI za Somalia na Djibout zimethibitisha kushiriki mashindano ya
riadha ya Afrika Mashariki na Kati kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20
yatakayofanyika nchini Aprili 29 na 30, imeelezwa.
Kaimu Katibu Mkuu wa Riadha Tanzania, Ombeni Zavalla (pichani kushoto) alisema kuwa tayari nchi hizo
zimethibitisha kushiriki kwa kuleta
majina ya wachezaji na viongozi wao watakaokuja nchini.
Mashindano hayo yatakayofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar
es Salaam, mbali na Djibout na Somalia, pia nchi zingine zinazotarajia
kushiriki ni Kenya, Uganda, Ethiopia, Zanzibar, Sudan, Rwanda na Burundi.
Alisema kuwa mashindano hayo kabla ya kufanyika yatatanguliwa na
mkutano wa viongozi wan chi shiriki, ambao utajadili maendeleo ya mchezo huo.
Aidha, timu ya taifa ya Tanzania Bara inaingia kambini kesho
katika shule za Filbert Bayi kujiandaa na mashindano hayo.
Awali, timu hiyo mara mbili ilishindwa kuanza kambi kutokana na
ukata na kusababisha makocha wake kuwa na hofu ya kutofanya vizuri.
Kocha Mkuu wa timu hiyo Robert Kalyahe alisema kuwa anahofu timu
yao kutofanya vizuri katika mashindano hayo baada ya kuchelewa kuanza mazoezi
wakati nchi zingine zilianza maandalizi mapema.
No comments:
Post a Comment