SIKU moja baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16
Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga imeangukia kwa Sagrada Esperanca ya
Angola katika michuano ya kuwania ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika.
Itakutana na Waangola hao katika hatua ya mtoano ambayo mshindi
wake ataingia hatua ya makundi ya michuano hiyo inayoshika nafasi ya pili kwa
ukubwa katika ngazi za klabu barani Afrika.
Kwa mujibu wa ratiba iliyopangwa na Shirikisho la Soka Afrika
(CAF) jana alasiri, Yanga baada ya kufungwa 2-1 na Ahly juzi usiku huko
Alexandria na hivyo kutolewa kwa jumla ya mabao 3-2, sasa itakipiga dhidi ya
timu hiyo inayomilikiwa na Shirika la Madini la Taifa la Angola.
Itaanza kwa kuwakaribisha Waangola hao kati ya Mei 6 na 8 jijini
Dar es Salaam na marudiano kuwa kati ya
Mei 17 na 18 nchini Angola.
Haijafahamika Angola zitachuana katika mji gani, ingawa Sagrada
iliyoanzishwa Desemba 22, mwaka 1976, yaani miaka 39 iliyopita, uwanja wake wa
nyumbani upo Dundo, katika Jimbo la Lund Norte ambao una uwezo wa kuingiza
mashabiki 3,000 kwa wakati mmoja.
Kama Yanga vile; timu ya Sagrada Esperanca ya Angola, ambayo itacheza na Yanga. |
Mshindi wa pili hupata dola 432,000 (sh milioni 907) wakati timu
zinazoshika nafasi ya pili na ya tatu katika kila kundi hupata dola 239,000 (sh
milioni 500) na ya mwisho katika kundi, yaani inayoshika nafasi ya nne, huambulia
dola 150,000 (sh milioni 315).
Wakati Yanga ikiangukia kwa Waangola, waliokuwa mabingwa watetezi
wa Ligi ya Mabingwa Afrika, TP Mazembe waliovuliwa ubingwa juzi, watakutana na Waarabu wa Tunisia, Stade
Gabesien, huku Esperance pia ya Tunisia iliyoitoa Azam FC ikipangwa kukutana na
Mo Bejaiaa ya Algeria.
Michezo mingine ya mtoani itakuwa kati ya Stade Malien (Mali) na
FUS Rabat (Morocco), Etoile du Sahel (Tunisia)
na CF Mounana (Gabon), Al-Ahli Tripoli (Libya) na Misr El-Makasa
(Misri), Al-Merreikh (Sudan) na Kawkab
Marrakech (Morocco), wakati Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini itacheza na
Medeama ya Ghana.
Yanga na timu nyingine zilizotolewa katika Hatua ya 16 Bora ya
Ligi ya Mabingwa Afrika, zimeangukia Kombe la Shirikisho kama Kanuni za CAF
zinavyoeleza kuwa, timu ambazo zitatolewa katika Raundi ya Pili ya Ligi ya
Mabingwa zitaangukia Kombe la Shirikisho kukutana na timu nane zilizosonga
mbele ambapo zitacheza mechi za mtoano za nyumbani na ugenini kisha
zitakazofuzu zitaingia hatua ya makundi.
No comments:
Post a Comment