Na Mwandishi Wetu
TIMU ya Al Ahly ya Misri imetua nchini leo alfajiri tayari kwa
pambano lao la Ligi ya Mabingwa wa Afrika dhidi ya Yanga litakalofanyika
Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Pambano hilo ni la hatua ya 16 bora, ambapo timu hizo zitarudiana
siku 10 zijazo nchini Misri ili kusaka timu itakayotinga hatua ya makundi.
Timu hiyo imekuja na wachezaji wakali 21 pamoja na kocha wao Martin
Jol, ambaye alianza kuifundisha timu hiyo mwezi uliopita baada ya kumwaga wino.
Kocha wa Al Alhy, MMartin Jol mara baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa JK Nyerere leo alfajiri. |
Kocha huyo wa Ahly amewaita wachezaji wake wote wakali ambao wamo
katika safari hiyo.
Pambano hilo linakumbushia lile la mwaka 2014, ambapo Yanga
waliibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza dhidi ya Al Ahly kabla
ya kufungwa bao kama hilo na kufanya mchezo huo kuamliwa kwa matuta, ambapo
Yanga ilifungwa 4-3.
Said Bahanuzi na Mbuyi Twitte ndio walioikosesha Yanga ushindi
baada ya kukosa penalti zao katika mchezo huo uliofanyika jijini Cairo, Misri.
Katika kikosi hicho, Jol amewaacha beki Mohamed Naguib, kiungo Saleh
Gomaa na Ahmed Hamdy, ambacho kimetua leo tayari kwa mchezo huo.
Mchezaji aliyepona hivi karibuni misuli, Sherif Ekramy ameitwa
baada ya kuwa nje ya uwanja tangu Februari,pamoja na kipa wa akiba Ahmed Adel akichukua
nafasi katika mechi zilizopita.
Al Ahly imetinga hatua ya 16 bora baada ya kuifungisha virago Recreativo
ya Angola kwa ushindi wa jumla ya mabao 2-0, wakati Yanga walipinya baada ya
kuifunga APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2.
Yanga walishinda mabao 2-1 katika mchezo wa kwanza uliofanyika
kwenye Uwanja wa Amavubi jijini Kigali, Rwanda kabla ya kutoka sare ya
kufungana 1-1 katika mchezo wa marudiano jijini Dar es Salaam.
Kikosi cha Ahly:
Makipa: Sherif
Ekramy, Ahmed Adel na Mosad Awad.
Mabeki: Ahmed Fathi,
Bassem Ali, Mohamed Hani, Saad Samir, Rami Rabia, Ahmed Hagazy na Sabri Rahil.
Viungo: Hossam
Ghaly, Hossam Ashour, Amr El-Sulaya, Ahmed El-Sheikh, Walid Soliman, Moemen
Zakareya, Ramadan Sobhi na Abdalla El-Said.
Washambuliaji: Malick Evouna, Amr Gamal na Emad Meteb.
Yanga wenyewe wako Chake Chake Pemba wakijifua kwa ajili ya
pambano hilo linalotarajiwa kuwa kali na la kuvutia huku Al Ahly wakitaka
kuendeleza makali yao na Yanga kulipa kisasi cha kutolewa mwaka 2014.
No comments:
Post a Comment