Meneja wa Kitengo cha Michezo cha Azam TV, Baruwan Muhuza akiwa ameshika Kombe la ASFC wakati wa kupanga ratiba ya mashindano hayo. |
Na Mwandishi Wetu
YANGA na Azam FC zote zimekataa kucheza Nusu Fainali ya Kombe
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports
Federations Cup (ASFC) 2016 Aprili 24.
Yanga itamenyana na Coastal Union katika Nusu Fainali ya michuano ya
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports
Federations Cup 2016.
Yanga watakuwa wageni wa Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani mjini
Tanga Aprili 24, mwaka huu, siku ambayo Azam FC itamenyana na Mwadui FC Uwanja
wa Mwadui Complex, Shinyanga.
Hiyo inafuatia droo iliyopangwa jana studio za Azam TV, wadhamini
wa michuano hiyo, Tabata, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Katibu wa TFF,
Selestine Mwesigwa.
Zote zimekuja na sababu sawa, kwamba zitakuwa na mechi za michuano
ya Afrika Aprili 20 ugenini na zinatarajia kurejea Dar es Salaam Aprili 21
usiku, hivyo watakuwa na muda mfupi kabla ya mechi za Kombe la TFF ambazo
watacheza ugenini.
Yanga watakuwa wageni wa Al Ahly mjini Alexandria Aprili 20,
katika mchezo a marudiano hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya
kulazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam Jumamosi iliyopita.
Wakati Azam FC watakuwa wageni wa Esperance mjini Tunis siku hiyo
hiyo, katika mchezo wa marudiano hatua ya 16 Bora Kombe la Shirikisho Afrika
baada ya Jumapili kushinda 2-1 jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya upangwaji wa droo ya Nusu Fainali ya michuano
hiyo studio za Azam TV usiku wa jana, Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba
alisema kwamba ratiba imekaa vibaya.
“Sisi
tutacheza
mechi Tunisia tarehe ya 20, ina maana kuondoka kule ni tarehe 21, tufike saa
ngapi Dar es Salaam na saa ngapi tupate ndege ya kwenda Mwadui?”alihoji Kawemba.
Ameishauri TFF
kuangalia uwezekano wa kusogeza mbele mechi hizo, ili kila timu ipate fursa ya kujiandaa
vizuri.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga,
Jerry Muro naye alisema kwamba watacheza mechi Misri Aprili 20 na wanatarajiwa
kurejea Dar es Salaam Aprili 21, wakati Tanga njia kuu ni basi.
“Ufike
Dar es Salaam tarehe 21, uondoke kwa basi Dar es Salaam tarehe 22 kwenda
Tanga kwa safari ya karibu nusu siku, kisha tarehe 24 ucheze mechi, hii ni
ngumu sana,”alisema
Muro.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa aliyekuwapo
kwenye droo hiyo aliwakatisha tamaa viongozi hao wa Yanga na Azam kwa kusema
kwamba hawaoni tatizo katika tarehe za Nusu Fainali.
Coastal Union iliingia Nusu
Fainali baada ya kuitoa Simba SC kwa kuifunga mabao 2-1, wakati Azam FC iliitoa
Prisons kwa kuifunga 3-1, Mwadui FC iliitoa Geita Gold kwa kufunga 3-0 na Yanga
SC iliwafunga Ndanda FC 2-1.
Bingwa wa Kombe la ASFC, michuano iliyoanza na timu 64 Novemba
mwaka jana, ataiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho
Afrika mwakani.
Katika hatua ya awali, kila timu ilipatiwa fedha za usafiri Sh
Milioni 3, na vifaa vya mashindano kutoka kwa wadhamini, Azam TV ikiwa ni
sehemu ya udhamini wa Bilioni 3.3, wakati bingwa atajinyakuliwa kitita cha Sh.
Milioni 50,
Fainali inatarajiwa kuchezwa wiki moja baada ya Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara kumalizika.
No comments:
Post a Comment