Na
Mwandishi Wetu
WIZARA
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeipongeza Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kwa kuchukua hatua za haraka za kudhibiti
ugonjwa wa Ebola usiingie nchini, imeelezwa.
Kauli
hiyo imetolewa leo na Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Ummy Mwalimu katika hotuba
yake kwa wananchi walioshiriki Matembezi ya Hiyari ya kuelimisha na kuhamasisha
Jamii kuzuia ugonjwa huo usiingie nchini yaliyoanzia kwenye viwanja vya Mnazi
Mmoja na kuishia Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam, ambapo imesharipotiwa
ugonjwa huo umeingia nchi jirani ya Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo.
Meneja Rasilimali Watu na Utawala wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, TAA, Abdi Mkwizu (mwenye fulana ya bluu) wakati wa matembezi hayo leo. |
Mhe.
Mwalimu amesema TAA inafanya jambo jema kwa kuhakikisha wasafiri wote
wanaoingia nchini kupitia viwanja vya ndege wanafanyiwa ukaguzi na kutoa
taarifa za afya zao kwa wale ambao watabainika kuwa na joto la mwili lisilokuwa
la kawaida.
“Nawapongeza
sana tena sana Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania kwa kuhakikisha nchi
inakuwa salama bila kupata maambukizi ya ugonjwa huu wa Ebola, imeripotiwa sasa
huu ugonjwa upo Kivu Kaskazini, ambapo ni karibu na nchini na Wavuvi wanakuwa na
muingiliano kwa kutoka huko na kuja nchini,” amesema Mhe. Mwalimu.
Hatahivyo,
amesema pamoja na ugonjwa huo kutoingia nchini, lakini kwa mujibu wa taarifa
kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), tayari imeripotiwa wananchi 111 wa Kongo
wamepata maambukizi na kati yao 75 sawa na asilimia 67 wamefariki, hivyo
inakisiwa endapo Tanzania ikiwa na wagonjwa 100 anaweza kusababisha vifo vya
watu 50.
"Ebola
bado haujaingia nchini Tanzania, lakini ni kweli kwamba tupo katika hatari
kubwa zaidi kupata ugonjwa huu, hii inatokana na mlipuko wa ugonjwa huu kuwepo
katika eneo la Kivu Kaskazini na imesharipotiwa kuua watu na sisi hatupo mbali
na eneo la Kivu, hivyo tusikubali ugonjwa huu kuingia nchini na tutoe elimu juu
ya ugonjwa huu,” amesisitiza Mhe. Waziri Ummy Mwalimu.
Aidha,
Mhe. Mwalimu aliwaomba Viongozi wa Dini kutumia majukwaa yao katika mahubiri
yao kutoa tahadhari kwa wananchi kuhusiana na ugonjwa huu wa Ebola, ambapo pia
awaomba wasanii wa muziki na viongozi wa Siasa nchini kutumia majukwaa yao ili kufikisha
taarifa kwa wananchi juu ya ugonjwa huu.
Naye
Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa TAA, Bw. Lawrence Thobias
aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu, Bw. Richard Mayongela amesema viwanja vya
ndege vimekuwa na mikakati ya muda mrefu kwa kushirikiana na Wataalamu wa Afya
ya kudhibiti magonjwa ya kuambukiza ukiwemo Ebola.
Bw.
Thobias amesema sasa viwanja vyote hususan vilivyopo katika mipaka ya nchi
zimefungwa mashine maalum (thermos scanner) za kutambua joto la mwili wa
binadamu, na ikibainika limezidi nyuzi joto 38, abiria huyo anapelekwa katika
chumba maalum na kufanyiwa mahojiano ya kina juu ya afya yake na pia abiria
wanaowasili na ndege zinazofanya safari nchi jirani na Kongo nao hunawa mikono
kwa dawa maalum kabla ya kutoka nje ili kuendelea na safari zao.
“Kwa
upande wetu tumeweka mikakati kamambe ili huu ugonjwa usiweze kuingia nchini,
mbali na abiria kunawa kwa dawa maalum anapoingia tu ndani ya mlango wa
wasafiri wanaotoka nje ya nchi, pia kuna mashine maalum (thermo scanners) ambazo
zinaonesha joto la mwili wa kila abiria anapoingia kwenye lango hilo, na
kimetekwa chumba maalum cha mahojiano kwa wale wanaobainika kuwa na joto la
juu, na pia katika hospitali ya Temeke napo kipo chumba maalum endapo
atabainika mgonjwa aliyepatikana kupitia viwanja vyetu anapelekwa huko,”
amesema Bw. Thobias.
Mbali
na kuweka mashine mbalimbali kwenye viwanja vya ndege nchini, pia TAA ikiwa ni
mmoja wa wadhamini imechangia Tshs. Milioni 5 kwa ajili ya kampeni ya kutoa
elimu juu ya ugonjwa wa Ebola kwa wananchi.
Ugonjwa
wa Ebola unasambazwa
na virusi vya Ebola na husababisha homa kali inayoweza kuambatana na kutokwa
damu mdomoni, puani, masikioni, machoni na sehemu nyingine za wazi na unaenea
kwa haraka, na namna ya kujikinga na ugonjwa huu ni pamoja na kuepuka kugusa
damu, machozi, jasho, matapishi, kamasi, mkojo au kinyesi cha mtu mwenye dalili
za ugonjwa; pia mtu hatakiwi kugusa, kuosha au kuzika maiti ya aliyekufa kwa
Ebola; pia usiguse au kula wanyama kama popo, sokwe au swala wa msituni.
Dalili
za Ebola ni pamoja na homa kali, maumivu ya kichwa na misuli, mwili kulegea,
kutapika, kuharisha, vipele na kutokwa damu maeneo mbalimbali ya mwili.
No comments:
Post a Comment