1.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya
Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (kushoto) akiongea na waandishi
kuhusiana na viwanja vya ndege kuchagiza uingiaji wa watalii nchini. Kulia na Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Prof.
Audax Mabula.
Mamlaka
ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imejipanga kupitia kaulimbiu yake `kuifungua
Tanzania kwa ulimwengu' kupitia sekta ya Utalii nchini, kwa kuimarisha usafiri
wa anga ili kuhakikisha watalii wote wanafikia vivutio vyote vya utalii kwa
haraka zaidi.
Hayo
yamebainishwa juzi na Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Richard Mayongela alipokuwa
akizumgumza na waandishi wa habari siku ya ushiriki wa Mamlaka katika Tamasha
la Urithi Wetu linaloanza leo Jumatatu (Oktoba Mosi, 2018) kwa Mkoa wa Dar es Salaam.
"Viwanja
vyetu vya ndege ndio milango mikuu wa watalii kupita, hivyo tupo hapa kuwaambia
wananchi, wadau pamoja na Jumuiya za Kimataifa kwamba sasa kuna fursa ya
kutanganza vivutio vya kitalii kupitia viwanja vyetu vya ndege kwa kuwa vinatumika
kwa usafiri wa anga lakini pia tunaweza kuvitumia kibiashara kwa kutangaza
vivutio vyetu" alisema Bw. Mayongela.
Bw
Mayongela pia amewapa wito Watendaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii kutangaza
vivutio vilivyopo kupitia Viwanja vya ndege lakini pia kuwaeleza wadau kwa njia
mbalimbali zilizopo Tanzania ili watalii wanapowasili waweze kupata picha
halisi ya maeneo ya kutembelea akiwa nchini.
Aidha
Bw. Mayongela ameongeza kwamba Mamlaka ina mtandao mkubwa na inasimamia viwanja
58 vilivyopo chini ya serikali, ambavyo vipo kila sehemu penye vivutio vya
utalii na wamejiimarisha kuhakikisha huduma bora ya usafiri wa anga.
"Sehemu
ya Kaskazini mwa nchi yetu ambapo ndio kuna vivutio vingi, vipo viwanja vya
ndege vya kutosha, tuna Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA),
Kiwanja cha Lake Manyara ambacho kimejengwa kwa mkakati wa kutumika kwa watalii
na kinafanya vizuri sana kwa kuingiza watalii wengi, vilevile tuna mpango wa
kujenga kiwanja kipya katika Mkoa wa Manyara,” alibainisha Bw. Mayongela.
Akizungumzia miundombinu ya Viwanja
vya Ndege kwa Kanda ya Kusini ameeleza kwamba serikali imejitoa kufanya
maboresho ya kiwanja cha Mtwara kwa lengo moja kuu la kuvutia watalii wengi
zaidi ili waweze kushuhudia vivutio vya utalii vilivyopo maeneo hayo.
“Serikali inaboresha kwa kufanya
upanuzi na ukarabati mkubwa wa Kiwanja Cha Ndege cha Mtwara, pamoja na sababu
za kiuchumi lakini pia lengo ni kuvutia watalii wengi zaidi ili waweze
kushuhudia vivutio vilivyopo, sio hivyo tu lakini pia Kilwa masoko tuna
kiwanja, Lindi tuna kiwanja, Nachingwea mpaka Masasi kote tuna viwanja” Alisema
Bw. Mayongela.
Akizungumzia upande wa nyanda za juu
Kusini Bw. Mayongela amebainisha kwamba baada ya ukarabati mkubwa kukamilika
kutakuwa na kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Songwe, Njombe mpaka Iringa
kutakuwa na viwanja vizuri vya ndege ili kuhakikisha kwamba vivutio vilivyopo
Tanzania vinafikika kwa urahisi.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi
Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Prof Audax Mabula ameeleza kwamba Tamasha la
Urithi Wetu lililobuniwa na Wizara ya Maliasili na Utalii lina madhumuni makuu
mawili ikiwemo ya kuwezesha kuonyesha fursa zote zinazoizunguka tasnia hii.
“Madhumuni makuu ni kuendeleza,
kutambua na kuhifadhi urithi wetu wa utamaduni kwa ajili ya kizazi kilichopo na
kinacho kuja lakini pili ni kubadili urithi wetu wa utamaduni kuwa zao la
utalii hayo ndio malengo makuu mawili” alisema Prof Mabula.
TAA wametoa msaada wa fulana 100 kwa
ajili ya washiriki wa tamasha la Urithi Wetu, ambalo litafikia tamati Oktoba 6,
2018 kwa kufungwa na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa.
Imeandaliwa
na Idara ya Uhusiano Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA)
No comments:
Post a Comment