1.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja
vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (kulia) akiwaongoza Wafanyakazi
wa Mamlaka hiyo, Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius
Nyerere (JNIA), Bw. Paul Rwegasha (katikati) na Ofisa Uhusiano, Bi. Bahati
Mollel (wapili kulia) kukabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya Sh Mil 5 Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Anne Makinda
(wapili kushoto) na Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya hafla hiyo, Mbunge wa
Muleba Kusini, Prof. Anna Tibaijuka. Hafla hiyo ilifanyika jana usiku kwenye
ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
MAMLAKA
ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imeunga mkono juhudi za Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kupitia Umoja wa Wabunge Wanawake wa Bunge hilo (TWPG)
kukusanya fedha kwa ajili ya kujenga vyoo salama vya shule nchi nzima kwa ajili
ya mtoto wa Kike kwa kutoa mchango wa kiasi cha Sh Mili 5.
Hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi
Mkuu wa TAA, Bw. Richard Mayongela, alikabidhi msaada huo wa fedha kwa mgeni
rasmi, Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Anne
Makinda.
Akizungumza
kwenye hafla hiyo iliyoudhuriwa na viongozi mbalimbali, wakiwemo Wabunge, Wakuu
wa Taasisi za Umma na Binafsi, Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai, aliwapongeza
Wabunge hao kwa hatua hiyo ya kuhakikisha kunakuwepo kwa mazingira bora shuleni
ili kutoa haki sawa ya kupata elimu kwa wanafunzi wa jinsia zote.
“Wazo
hili litasaidia sana serikali katika kuhakikisha mazingira ya shule
yanaboreshwa ili kutoa nafasi sawa kwa wanafunzi wote wa kike na kiume,” alibainisha
Spika Ndugai.
Alisema
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli,
amefurahishwa na kitendo hicho na kwamba ameshindwa kuhudhuria hafla hiyo kwa
vile bado yupo kwenye msiba wa dada yake huko Chato mkoani Geita.
Kwa
upande wake, mgeni rasmi Mhe. Anne Makinda aliwapongeza Wabunge hao wanawake
kwa hatua hiyo ya kuunga mkono juhudi za serikali na kuwataka Wabunge wanaume
kuwaunga mkono wenzao katika kufanikisha kampeni hiyo inayolenga kukusanya
kiasi cha shilingi bilioni 3.5 zitakazowezesha kujenga vyoo salama vya shule
kwenye majimbo yote 264 nchi nzima.
Taasisi
Mbalimbali zilichangia kwenye harambee hiyo, ambapo pia vitu mbalimbali vilinadiwa
na fedha zitakazopatikana zitakwenda kufanya kazi ya
ujenzi huo.
No comments:
Post a Comment