Monday, 10 September 2018

TAA Waanza Kugawa Viwanja Kufidia Wakazi wa Kipunguni Ili Kupisha Upanuzi wa JNIA


Wananchi wakiwa katika ofisi ya mtendaji wakisubiri maelezo kuhusu upimiwaji wa viwanja Mtaa wa Kidole  Kata ya Msongola

Na Mwandishi Wetu

MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Manispaa ya Ilala, vOfisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala na Kampuni ya Tanzania Remix imeanza kutekeleza agizo la Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi), Mhandisi Atashasta Nditiye juu ya ulipaji wa fidia ya viwanja kwa Wananchi wa Kata ya Kipunguni A na Kipunguni Mashariki.

Agizo hilo alilolitoa Agosti 30 mwaka huu, limeanza kutekelezwa leo  kwa Wananchi watokao Kipunguni Mashariki na Kipunguni A kwenda  mtaa wa Kidole na Luhanga kupewa viwanja 537 ndani ya Kata ya Msongola ili kupisha mradi wa upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius  Nyerere (JNIA).


Zoezi la upimaji likiendelea ili kuweza kuonyesha mawe ya upimaji kabla ya kumkabidhi Mwananchi husika mapema leo katika Mtaa wa Kidole kata ya Msongola
Awali, Mhandisi Nditiye alitoa maagizo kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege  Bw, Richard Mayongela kushirikiana na Manispaa ya Ilala, Mkuu wa Wilaya na Kampuni ya Tanzania Remix, ambayo ilihusika na upimaji wa maeneo hayo kuhakikisha inawagawia wananchi viwanja hivyo na kuhakikisha viwanja hivyo vina ubora.

“Mshirikiane na Tanzania Remix na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Manispaa  kuwagawia Wananchi viwanja hivi vilevile  shirikianeni na  vyombo vya ulinzi na usalama kuwabaini  wafanyakazi wote wa TAA waliojiingiza kwenye mradi huu na kujipatia viwanja kinyume na utaratibu wakati hawahusiki na mradi huu, wabainishwe na wachukuliwe hatua kali za kisheria,” alisema.

Mmoja wa Wananchi kutoka Kipunguni ambaye ameoneshwa eneo lake akiwa amepiga picha katika eneo hilo  Mtaa wa Kidole kata ya Msongola mapema leo.
Safari Kishiwa na Evaline Malume ni miongoni mwa wananchi walioanza kugawiwa viwanja hivyo na kuishukuru Serikali kutokana na maeneo hayo kuwa katika mazingira mazuri.

Wananchi hao walidai wanawashangaa baadhi ya wananchi wenzao walioathiriwa na mradi huo kukimbilia mahakamani kwasababu mbalimbali  zisizo na mashiko.
"Tuwaombe tu wenzetu wafute kesi waje wachukue viwanja, viwanja hivi vipo kwenye mazingira mazuri tofauti na wanavyofikiri," walisema.

Baadhi ya Wananchi wa Kipunguni Mashariki na Kipunguni A wakiwa na Maofisa wakisubiri kupimiwa maeneo yao katika Mtaa wa Kidole kata ya Msongola mapema leo.
Wapima ardhi Masasu Magenyi (Manispaa ya Ilala) na Hemedi  Fundi  (Tanzania Remix) wakisoma ramani za eneo hilo wakati wa kugawa maeneo hayo kwa Wananchi Mtaa wa Kidole Kata ya Msongola Wilaya ya Ilala mapema leo.


No comments:

Post a Comment