Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano sekta ya Uchukuzi Mhandisi Atashasta Nditiye akiwa katika ofisi ya Mkurugezi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, TAA, Richard Mayongela. |
Na Mwandishi Wetu
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano sekta
ya Uchukuzi Mhandisi Atashasta Nditiye, akiongozana na Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Bw. Richard Mayongela leo wamefanya
ziara katika mtaa wa Luhanga, Kata ya Msongola wilaya ya Ilala, eneo ambalo
wananchi wa Kipunguni A na Kipunguni Mashariki wanapewa viwanja ili kupisha upanuzi wa Kiwanja cha ndege cha
Julius Nyerere (JNIA).
Katika ziara hiyo Naibu Waziri Nditiye alipokelewa na
malalamiko ya kutokulipwa fedha za fidia kutoka kwa wamiliki wa mashamba kabla
ya upimaji wa viwanja katika mtaa wa Luhanga ambavyo ndivyo vinavyotakiwa kugaiwa kwa wananchi wa Kipunguni A na
Mashariki.
Akiwasilisha malalamiko yake kwa Mhandisi Nditiye,
mmoja wa wamiliki wa viwanja katika eneo la Luhanga, Bw. Mrisho Hashim
Kawete alieleza kwamba mkataba
unaelekeza kwamba ndani ya miezi minne walipaswa kuwa wamelipwa pesa zao zote
lakini mpaka sasa, hilo halijatekelezwa.
“Kwa mujibu wa mkataba tulitakiwa kupewa malipo yetu
ndani ya miezi minne tangu kusainiwa kwa mkataba lakini mpaka leo hii
tunashangaa wanakuja watu wengine kupewa viwanja kabla hatujamaliziwa malipo
yetu”, alisema Bw. Hashim.
Akiwasilisha pia malalamiko yake kwa Naibu Waziri
Aliyekua mjumbe wa Luhanga katika
kipindi mchakato unaanza Bw. Elisante Kisingo Mmwiri ameeleza kwamba mradi huo
wameupokea kwa mikono miwili lakini inawakatisha tamaa kuona kama ndani yake
kuna ajenda za siri.
“Kwa kweli tunashindwa kuelewa mkutano huu una ajenda
gani ya siri, maana hata wananchi hawapewi taarifa juu ya ujio wa Viongozi,
mradi huu tumeupokea na tunapenda maendeleo lakini kuna vikwazo vingi sana
katika huu mradi”, alisema Bw. Mmwiri.
Naye mwakilishi wa Kampuni ya Tanzania Remix ambayo
ndio imepewa jukumu la kusimamia upatikanaji na ugawaji wa viwanja kwa wakazi
wa Kipunguni, Bw. Lwembu Henjewele ameeleza kwamba kutokana na uwepo wa
asilimia arobaini na asilimia sitini tayari kuna mgawanyo, mfano kama mtu ana
viwanja kumi basi vinne vya Tanzania Remix sita vya kwake na huyo hastahili
kulipwa fidia isipokua kama anakubali sehemu ya viwanja vyake sita vilivyo
bakia viingie kwenye mauzo basi atastahili kupata fedha yake inayotoka kwenye
mauzo.
Baada ya Malalamiko hayo Naibu Waziri Nditiye ametoa
maagizo kwa Mkurugenzi Mkuu wa TAA kwamba ndani ya wiki moja atarejea tena kuja
kuangalia viwanja na asikute migogoro katika eneo hilo.
“Mimi nakupa wiki moja na leo ni Jumatatu, mimi
nitakuja jumatatu tena ili tuwe na uamuzi wa mara moja ili tuweze kuwakamata
hawa watu wa Tanzania Remix kama watashindwa kutuonesha viwanja visivyokua na
Mgogoro 537”, alisema Naibu Waziri Nditiye.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TAA ameeleza kwamba
ameyapokea maelekezo ya Naibu Waziri na kwamba Mkataba umeshaisha muda wake
hivyo utekelezaji wake utafanyika ndani ya kipindi cha wiki moja.
“Ndani ya wiki moja kama atakua hajatekeleza maagizo
haya yaliyotolewa basi hakutakua na njia nyingine zaidi ya kuchukua hatua za
kisheria ikiwepo kudai viwanja ambavyo tulikua tunahitaji, pia napenda
kusisitiza kwamba hatupendi kuona wananchi wanapata shida hivyo wananchi
watambue kwamba hatujawaacha na kwamba tutashirikiana mpaka mwisho, hakuna haki
ya mwananchi itapotea kila mtu atapata haki yake” alisema Bw. Mayongela
Mkataba kati ya Tanzania Remix na Mamlaka ya viwanja
vya Ndege TAA ulisainiwa tarehe 28 mwezi Mei mwaka 2014 na ukomo wake ukiwa
tarehe 27 mwezi Aprili 2015, ambapo malipo yalifanyika kwa awamu mbili, ya
kwanza ikiwa ni Pesa za kitanzania milioni 700 na awamu ya pili pesa za
kitanzania bilioni 3.
No comments:
Post a Comment