Na Mwandishi Wetu
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara, Simba
wamefungwa bao 1-0 dhidi ya Mbao katika mchezo uliochezwa leo kwenye Uwanja wa
CCM, Kirumba jijini Mwanza.
Ni mchezo wa kwanza Simba inapoteza tangu kuanza kwa
msimu huu, lakini pia, rekodi yake ya kuifunga Mbao ikivunjwa.
Mbao ilipata bao hilo dakika ya 26 likifungwa na Said
Khamis kwa mkwaju wa penalti baada ya Pastory Athanas kuzuiwa na kipa Aishi
Manula alipokuwa akijaribu kufunga.
Kwa ushindi huo, Mbao unaisogeza hadi kileleni mwa
msimamo wa ligi kwa pointi 10 ikifuatiwa na Yanga yenye pointi tisa, JKT tisa,
Azam nane na Simba ikiwa katika nafasi ya tano kwa pointi saba.
Wekundu hao wa Msimbazi walimiliki mpira kwa dakika
90 na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga, lakini walishindwa kuzitumia
kutokana na ukuta uliowekwa na wapinzani.
Kocha Patrick Aussems wa Simba alifanya mabadiliko
kadhaa ya wachezaji akiwatoa Mohamed Ibrahim, Shiza Kichuya na kuingia Meddie
Kagere na Rashid Juma lakini bado haikusaidia.
Mbao walicheza muda wote kwa kujihami na kuwaacha
wachezaji wachache kushambulia kwa kushtukiza lakini walishindwa kuzitumia
baadhi ya nafasi walizokuwa wakizipata ili kuendeleza mabao.
Rekodi zinaonesha tangu Mbao ipande Ligi Kuu
haijawahi kuifunga Simba. Msimu wa 2016/2017
wekundu hao walivyokuwa nyumbani waliifunga bao 1-0 na kwenye Uwanja wa
Kirumba walishinda 3-2.
Pia, msimu wa 2017/2018 Simba ugenini ilipata sare ya
mabao 2-2 na nyumbani ilishinda 5-0.
Mechi nyingine zilizochezwa jana ni African Lyon
iliibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Singida United naTanzania Prisons
ikilazimishwa sare nyumbani ya mabao 2-2 dhidi ya Kagera Sugar.
No comments:
Post a Comment