Na Mwandishi Wetu
ASASI ya Pakacha Group imepongezwa kwa kutoa elimu
kwa wananchi juu ya ufuatiliaji wa miradi ya maji na utekelezaji wake ili
kuondokana na shida ya maji katika maeneo yao.
Wakizungumza katika mkutano wa siku moja uliondaliwa
hivi karibu na Pakacha Group kwa ufadhili wa The Foundation For Civil Society,
wananchi wamesema ongezeko la idadi ya watu na ujenzi holela wa makazi ni
miongoni mwa changamoto zinazopelekea
ukosefu wa upatikanaji wa huduma za maji kwa wananchi.
Washiriki wa mkutano huo walikuwa wananchi wa Kata tatu
za Kwembe, Kibamba na Msigani, viongozi wa serikali za mtaa, watendaji,
madiwani na wakuu wa idara ya maji kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.
Adam Kingu, mjumbe wa serikali ya mtaa wa Malamba
Mawili amesema Pakacha inafanya kazi nzuri, huku akiwaomba viongozi wa serikali
za mitaa watoe elimu ili kuzuia ujenzi holela ambao umepelekea uharibifu wa
miundombinu ya maji.
“Watu wamejenga bila kufuata utaratibu hivyo ni
rahisi miundombinu ya maji kuharibiwa”, amesema
Kingu.
Everyline Francis, mjumbe wa kamati ya maji ya Kata
ya Kwembe amesema jamii ipewe elimu ya kutunza vyanzo vya maji na kuzuia
uharibifu wa mazingira.
Upatikanaji wa maji umekuwa na changamoto katika kata
za Kwembe, Msigani na KIbamba, hivyo asasi ya Pakacha, kwa ufadhili wa The
Foundation For Civil Society kulazimika kutoa elimu kwa wananchi juu ya
ufuatiliaji na utunzaji wa vyanzo vya maji.
Diwani wa Kata ya Kwembe wilayani Ubungo, Dweza
Kolimba amesema asasi za kiraia kama Pakacha zina nafasi kubwa ya kuleta
maendeleo katika jamii kwa kushirikiana na wananchi na watendaji wa serikali.
Akizungumza katika semina hiyo kwa ajili ya kujadili
utatuzi wa changamoto ya maji, kuanzia ufuatiliaji wa rasilimali fedha na utekelezaji
wake, Kolimba amesema upatikanaji wa maji katika kata yake umekuwa wa shida
huku akisema kuwa wananchi wengi watapata maji baada ya mradi mkubwa wa
Luguruni kukamilika.
“Tayari mabomba yamesambazwa, hivyo tunaomba mradi
huu uishe mapema ili watu wapate maji,” amesema Kolimba.
Akizungumza kwa niaba ya Mhandisi wa maji wa Manispaa
ya Ubungo, Hamad Sendekwa amesema ameomba wananchi washirikiane na watendaji
ili kutatua kero za maji na jitihada zinaendelea kuhakikisha huduma hiyo muhimu
inapatikana wakati wote. Alisema ushirikiano huo utasaidia kuibua changamoto
zinazokwamishwa na rasilimali fedha au kutowajibika kwa baadhi ya watendaji.
Alisema asasi zinaweza kuleta mabadiliko kwa
kufuatilia miradi ya maji, ambayo inakwamishwa kwa sababu mbalimbali na
kuwaelimisha wananchi jinsi ya kulinda miundo mbinu ya maji na ufuatiliaji
wake.
Katibu wa Pakacha, Haroun Jongo amesema lengo la
mkutano huo ni kutoa msukumo kwa utelekezaji wa miradi kwa kuibua hoja kwa
wananchi, kwa lengo moja tu, kuleta maendeleo.
Amesema lengo lingine la mkutano huo lilikuwa kuleta
jukwaa la majadiliano kati ya viongozi, wananchi na watendaji wa serikali za
mitaa ili kutatua kero za maji kwa wananchi kupitia mfumo wa Pets.
Pets ni mfumo unaowezesha ufuatiliaji matumizi ya
rasilimali za umma zinazotoka Serikali Kuu au halmashauri kwa maendeleo ya
wananchi kuanzia ngazi za mitaa hadi kata na kuendelea.
No comments:
Post a Comment