Jengo la Tatu la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA Terminal 3) linavyoonekana kwa mbele. |
Na Mwandishi Wetu
NAIBU Waziri Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta
ya Ujenzi), Mhe. Elias Kwandikwa, amewataka wasimamizi na wakandarasi
wa mradi wa ujenzi wa jengo la tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha
Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TB3), kumaliza kwa wakati kama inavyoelezwa
kuwa ni Mei 2019.
Mhe. Kwandika ametoa kauli hiyo leo alipokamilisha
ziara yake ya kukagua maendeleo ya mradi huo, ambao imeelezwa umeshafikia
asilimia 83 kukamilika.
“Nimejionea mradi unaendelea vizuri kwani mara
ya mwisho nilipita hapa wakati ukiwa na asilimia 56 lakini sasa maendeleo
ni makubwa, lakini ninasisistiza mradi uishe kwa wakati ili uweze kutoa
huduma bora kwa abiria, kwani ninauhakika watakuwa wengi tofauti na
jengo la pili la abiria,” amesema Mhe. Kwandikwa.
Hatahivyo, amesema mkandarasi anaendelea kulipwa
kulingana na madai yake kila anapowasilisha cheti cha madai na madeni
wanayoidai serikali wataendelea kulipwa kwa kufuata taratibu.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege
Tanzania (TAA), Richard Mayongela amesema Mamlaka inaishukuru serikali
kwa ujenzi wa jengo hilo, ambalo litatatua kero ya msongamano kwenye
jengo la sasa.
“Tunalipokea jengo hili kwa mikono miwili na tunaishukuru
sana serikali kwa miradi mbalimbali ya viwanja vya ndege,” amesema
Mayongela.
Hatahivyo, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi
kuchangamia fursa za uwekezaji kwenye jengo la tatu la abiria na viwanja
vingine vya ndege, ambapo kunamaeneo ya migahawa, maduka ya bidhaa mbalimbali
vikiwemo vito na huduma ya usafiri.
Pia amewaaasa wananchi kuacha tabia ya kuvamia maeneo
ya viwanja vya ndege kwa kufanya makazi na kufanya shughuli nyingine
za kibinadamu kwa kuwa ni hatari kwa usalama.
Awali mmoja wa Wahandisi Wasimamizi wa JNIA-TB3,
Mhandisi Barton Komba amesema mradi umekamilika kwa asilimia 73 upande
wa jengo, huku asilimia 75 upande wa maegesho ya magari na asilimia
92 kwenye maegesho na viungio vya ndege.
Hatahivyo, Mhandisi Komba amesema mradi unakumbwa
na changamoto ya mkandarasi na Mhandisi Mshauri kutolipwa kwa wakati,
hali kadhalika kutorudishiwa kwa kodi kiasi cha Euro. 4,904,000 ambapo
awali kulikuwa na msamaha wa kodi, lakini sasa sheria imebadilika anapaswa
kulipa.
Mkandarasi wa mradi huo wa Kampuni ya BAM International,
Bw. Wolfgang Marchick amesema pamoja na mradi huo kuajiri Watanzania
asilimia 95 lakini bado wamekuwa wakikumbwa na changamoto ya kulipa
kodi, ambayo imekuwa ikiwaumiza.
Jengo hilo likikamilika litakuwa na uwezo wa kuhudumia
abiria milioni sita (6) kwa mwaka.
No comments:
Post a Comment