Wednesday 28 February 2018

Wanadamu Watakiwa Kujiandaa Kabla ya Kifo


  Mchungaji Augustino Simalenga wa Kanisa la TAG Kivule leo maeneo ya Kitunda akiombea mwili wa marehemu Jerome Swai aliyekuwa Fundi Sanifu Mkuu wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), kabla ya kusafirishwa kwa mazishi yatakayofanyika kesho wilayani  ya Rombo.

Na Mwandishi Wetu
MCHUNGAJI wa Kanisa la TAG Kivule, Augustino Simalenga amewataka wanadamu kujiandaa na kumrudia muumba wao, kwani hawajui siku wala saa watakapokufa.

Alitoa kauli hiyo leo kwenye misa ya kumuaga marehemu Jerome Swai aliyekuwa Fundi Sanifu Mkuu wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), iliyofanyika nyumbani kwake maeneo ya Kitunda, ambapo amewataka watu kujiandaa mapema kwa kuwa hawajui watakapokwenda baada ya kifo.

   Msemaji wa familia ya marehemu Jerome Swai aliyekuwa Fundi Sanifu Mkuu wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Silvester Shayo (kulia) akitoa shukrani  kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Wafanyakazi wa TAA na watu wote walioshiriki kwenye msiba huo. Marehemu Swai atazikwa kesho wilaya ya Rombo.

 “Neno la Mungu linatukumbusha kuwa tujiandae mapema, ndugu yetu Jerome ameshamaliza kazi, tunatakiwa kujitafakari sisi hatima yetu itakuwaje, kwani wapo waliolala mauti Biblia inasema hao wanapumzika wakisubiri siku atakaporudi Mwana wa Adam atakuja kuwachukua wote waliohai na wale waliokufa wakimuamini Kristu watafufuliwa kwanza ili kwa pamoja wamlaki Bwana wao mawinguni,” alisema Mchungaji Semalenga.

Alisema kila mtu atafakari maisha ya hapa duniani kwani mlango wa kutokea hapa duniani aidha ni kifo au siku Bwana atakapokuja kuchukua watu wake, hivyo ni vyema kujiandaa kwa kutafakari maisha baada ya hapa kwa sasa kuanza kujitengenezea hazina mbinguni.


Ofisa Utumishi Mkuu wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Priscus Mkawe akisoma wasifu wa marehemu Jerome Swai aliyekuwa Fundi Sanifu Mkuu wa JNIA, kabla ya kuagwa nyumbani kwake Kitunda na kusafirishwa kwenda Rombo kwa mazishi yatakayofanyika kesho.

“Ukisoma kitabu cha Mhubiri sura ya 3 utaona Mungu ameweka kila kitu na wakati wake, upo wakati wa kula na wakati wa kusema, wakati wa kunyamaza, wakati wa kuzaliwa na wakati wa kufa kila kitu kinawakati hata sisi tuliohai ni wakati wetu kuwa hai bali utafika wakati hatutaweza kuwa hai siku zote, na kila jambo lina mwanzo na mwisho, lakini mwisho wa jambo unatengenezwa wakati wa sasa kama maisha yetu ya sasa hatufikiri mwisho basi tukifika mwisho tutakuwa watu wa kujuta, watu wa kuomboleza na lakini sasa Mungu anatupa nafasi ya kuyakabili mambo yanayokuja na hatima ya maisha yetu,” alisisitiza.

Alisema katika kitabu cha Zabuni, kinasema binadamu amepewa maisha mafupi na machache, na kuishi ni miaka 70 na wachache wanaweza kuishi zaidi ya hiyo, ambapo ni tofauti na wanadamu wa kwanza waliishi miaka 100 ambayo nayo yalikuwa mafupi. Hata hivyo alisema baada ya kifo yapo maisha ya milele, ambayo mwanadamu anatakiwa kuyatafakari sasa kwa kujiwekea hazina itakayomwezesha kuishi vyema mbinguni.


 Kaimu Mkurugenzi wa  Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Johannes Munanka akiaga mwili wa aliyekuwa Fundi Sanifu Mkuu wa JNIA, Bw. Jerome Swai, ambaye atazikwa kesho wilayani Rombo.

Mchungaji Simalenga alisema amefanya utafiti katika huduma anazotoa lakini amegundua hakuna mwanadamu anayetaka kwenda jehanamu, hata asiyefanya ibada kwa Mungu anamatumaini ya kwenda mahala pema peponi.

“Mungu ameweka utaratibu na Mwanadamu akiuufuata ndio atafikia kwenye ule mpango ambao Mungu ameuweka, sasa kama hataki kuufuata anajikuta siku za maisha yake atajikuta mahala asipotaka kwa kilio, kujuta na kuomboleza, kwani alikuwa akipuuzia na kuona mambo ya Kimungu ni ya kiduni na watu maskini na wachini, wakati ni mambo ya msingi kuliko kitu chochote duniani,” alisema Mchungaji Simalenga.    

 Bi. Honoratha Emmilian ambaye ni mke wa marehemu Jerome Swai aliyekuwa Fundi Sanifu Mkuu wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), akilia kwa uchungu wakati wa kuuaga mwili wa mumewe nyumbani kwake Kitunda. Marehemu atazikwa kesho wilayani Rombo.

Naye Ofisa Utumishi Mkuu wa JNIA, Bw. Priscus Mkawe alisema marehemu Swai ameacha pengo kubwa kutokana na umahiri wake katika utendaji kazi wake uliotukuka.

“Marehemu Swai alikuwa mmoja wa wafanyakazi wa kipekee aliyefanya kazi kwa bidii na kujituma na kutokana na uchapakazi wake aliwahi kuchaguliwa kuwa mfanyakazi hodari kuanzia mwaka 2001, 2003 na 2017, hivyo JNIA na TAA kwa ujumla tumempoteza mfanyakazi hodari sana,” alisema Priscus.
Ndugu wa marehemu Jerome Swai wakiuaga mwili wa mpendwa wao leo nyumbani kwake Kitunda, ambapo anatarajiwa kuzikwa kesho wilayani Rombo. Swai alikuwa Fundi Sanifu Mkuu wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).
  Mkurugenzi wa zamani wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Prosper Tesha (mwenye miwani mbele) akijumuika na waombolezaji kwenye msiba wa aliyekuwa Fundi Sanifu Mkuu wa Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Jerome Swai aliyefariki Jumatatu ya wiki hii na atazikwa kesho wilayani Rombo.
Jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Fundi Sanifu Mkuu wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Jerome Swai likipandishwa ndani ya basi tayari kwa safari ya kwenda Rombo kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika kesho. Marehemu aliajiriwa mwaka 1984.



No comments:

Post a Comment