Tuesday, 13 February 2018

Real Madrid Uso kwa Uso na PSG Mabingwa Ulaya


MADRID, Hispania
MABINGWA wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya Real Madrid wamekamilisha kipindi chao cha mazoezi na leo watacheza dhidi ya Paris Saint Germain (PSG) katika mchezo wa kwanza.

Mchezo huo ni muhimu sana kwa Real Madrid kwani utaonesha mwelekeo wa mabingwa hao watetezi kama wataendelea kuwepo katika mashindano hayo au watatupwa nje.

Tayari Madrid ina rekodi ya mashindano hayo, ambapo mbali nakutwaa mara nyingi taji hilo zaidi ya timu nyingine, lakini pia timu hiyo ndio pekee iliyowahi kulitwaa taji hilo mara mbili mfululizo.

Nahodha wa Real Madrid na timu ya taifa ya Hispania, Sergio Ramos amewataka mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi leo kuishangilia timu hiyo.

Ramos aliandika kupitia katika mitandao ya kijamii akiwataka mashabiki hao kujitokeza kwa wingi kuiunga mkono timu hiyo itkapocheza dhidi ya Paris Saint Germain.

Naye kipa wa timu hiyo, Keylor Navas alisema kuwa PSG ni timu kubwa, lakini wanaamini katika kiwango chao.

“PSG ni timu kubwa, lakini sisi tunaamini katika kiwango chetu, “alisema Navas.
"Najisikia vizuri na ni jambo zuri sana. Msimu huu tulikuwa na baadhi ya mambo mazuri na baadhi sio mazuri. Hiyo ni sehemu ya soka.”

Alisema kuwa kucheza Ligi ya Mabingwa wa Ulaya ni ndoto ya kila mchezaji hapa. Kushinda taji la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya ni kitu fulani kizuri, ni faida kutwaa taji.

Katika mchezo mwingine wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya leo, Porto ya Ureno itaikaribisha Liverpool katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Dragão.

No comments:

Post a Comment