WAANDAAJI wa muda mrefu wa shindano la Miss Tanzania Kampuni ya
Lino Agency wametangaza kuachia ngazi kwa kutojihusisha tena na shughuli hizo za
urembo.
Tangu mwaka 1994 Lino imekuwa ikiandaa shindano hilo kwa
mafanikio lakini kuanzia mwaka juzi ilishindwa na kukumbwa na kashfa kadhaa
ikiwemo kumpa taji mrembo asiye na sifa na kushindwa kutoa zawadi kwa washindi
hali iliyofanya kufungiwa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata).
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Lino, Hashim
Lundenga ‘Uncle’ alisema wameamua kuachana na shughuli hizo tangu Februari 13,
mwaka huu na kuiachia Kampuni ya Look chini ya Mkurugenzi wake Miss Tanzania
mwaka 1998, Basila Mwanukuzi.
“Sababu kubwa ya kuacha shughuli hizi ni pamoja na malengo yetu
mapya ya kuachia damu changa waendeleze na kuleta chachu ili kuifanya Miss
Tanzania iwe juu… ili tusije kupata balaa zaidi tumeamua kumpa mwingine jukumu
hili,” alisema.
Lundenga alisema wamejitathmini na kuona kuwa kwa siku za
karibuni walishindwa kuandaa shindano hilo kutokana na changamoto mbalimbali
ingawa pia, wanajivunia baadhi ya mafanikio ikiwemo kuwahi kumtoa mrembo wa
dunia aliyeingia sita bora na kuitangaza nchi kimataifa.
Kwa upande wake, Mwanukuzi alisema anawashukuru Lino lakini pia,
waandaaji wa Miss Dunia kwa kumpa kibali kuwa ndiye muandaaji na kuahidi
kurudisha heshima ya shindano hilo.
“Tunatambua kumekuwepo na changamoto nyingi hivi karibuni katika
uandaaji chini ya Lino, sisi kama Look tumeziona, tumejiandaa kikamilifu na
tunaahidi kuboresha na kukuza yarudi katika hadhi yake kwa kuzingatia kanuni
zilizowekwa,” alisema.
Alisema watazindua rasmi shindano hilo mwishoni mwa mwezi huu na
kuanza mchakato, wakitarajia kupeleka mrembo katika mashindano ya dunia baadaye
mwaka huu.
Alisema kupitia mashindano ya mwaka huu wanataka kufanya
uchunguzi kujua ni kitu gani wanatakiwa wafanye kufikia vigezo vya kimataifa au
kama kuna figisu au siasa zinatumika wajue nini cha kufanya kwa lengo la
kuboresha.
Kwa upande wake, Katibu
Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza alisema kama serikali hawana budi
kuishukuru Lino kwa kusaidia vijana wengi wa kike kupata ajira kupitia fani
hiyo ya urembo.
“Ni imani yetu shindano lipo mikononi mwa mtu ambaye alipitia
kwenye urembo, ni kweli kuna changamoto lakini anaweza kuzigeuza na kuzifanya
fursa ili kurudi katika hadhi yake,” alisema na kuhimiza wazazi kutokuwa na
wasiwasi tena juu ya shindano hilo.
No comments:
Post a Comment