Monday, 20 August 2018

RC Pwani Afungua Mafunzo ya Mpira wa Meza leo


 
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo (watatu kulia) akiwa na viongozi wa kamati ya Olimpiki (TOC) na wale wa Chama cha Mpira wa Meza Tanzania pamoja na washiriki wa mafunzo ya ufundishaji mchezo wa mpira wa meza yanayoendelea Mkuza Kibaha.

Mwandishi Wetu, Kibaha

SERIKALI imesema kuwa itajitahidi kuuendeleza mchezo wa mpira wa meza katika shule zilizopo mkoani Pwani.

Hayo yalisemwa leo na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Everest Ndikilo wakati akifungua mafunzo kwa walimu wa mchezo wa mpira wa meza yanayofanyika katika shule za Filbert Bayi na kuhudhuriwa na washiriki 25 wanaofundishwa na mkufunzi kutoka Afrika Kusini, Clement Meyer.

Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi.

Ndikilo alisema kuwa atawasiliana na baadhi ya wawekezaji waliopo mkoani mwake ili kusaidia kukuza mchezo huo mkoani mwake, ombi ambalo alisema kuwa halitakataliwa.

Alisema bila shaka wawekezaji hao hawatashindwa kumpatia meza 100 na vifaa vingine kwa ajili ya kuuendeleza mchezo huo katika shule mbalimbali za mkoani Pwani.

Mkufunzi wa mafunzo ya ufundishaji wa Mpira wa Meza, Clement Meyer wa Afrika Kusini.

 Alisema kuwa elimu watakayopata walimu hao kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania, itasaidia kuwaandaa wachezaji watakaoweza kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.

Makamu wa Rsis wa TOC, Henry Tandau.

“Endapo nchi yetu itakuwa na walimu wengi wa mchezo wa Mpira wa Meza, na wakatawanywa kwenye shule zetu, ambapo ndiyo kwenye vipaji, basi miaka michache ijayo tunaweza kuwa na uwakilishi mzuri katika Michezo ya Kimataifa," alisema Ndikilo.

Makamu wa Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Henry Tandau aliwataka viongozi wa michezo nchini kuandaa mpango mkakati kabla ya kuomba fedha kwa wafadhili mbalimbali.

Alisema kuwa TOC imekuwa ikipata shida sana kupata mipango mikakati ya vyama au mashirikisho ya michezo, licha ya kamati hiyo kuvitaka vyama kuwasilisha mipango mkakati yao,

Katibu Mkuu wa TOC alisema mchezo wa Mpira wa Meza pamoja na kuwa mkongwe hapa Tanzania, bado vyama vya mchezo huo vya Tanzania Bara na Zanzibar, TTTA na ZTTA wana kazi ya ziada kuueneza katika mikoa mbalimbali nchini, kuliko kuchezwa Dar Es Salaam, na Zanzibar tu.

Alisema katika akili ya kawaida chama cha Kitaifa maana yake ni nchi nzima na siyo sehemu ya nchi kama inaoonekana kwa sasa. Hata hawa wanamichezo wanaotuwakilisha katika mashindano ya Kitaifa na Kimataifa wametoka Mikoani.

 
Alisema kuna jinsi ya kuwapata wanamichezo bora wa mpira wa meza walioko Mikoani kama kuandaa mashindano ya Mikoa ambayo kwa sasa tangu awe Katibu Mkuu TOC hajawahi kusikia yakifanyika. Vile vile jitihada za ziada zifanyike kwa mchezo wa mpira wa meza kuenezwa katika shule zetu, ambapo ndipo penye vipaji.








No comments:

Post a Comment