Sunday, 12 August 2018

Mahakama Yazuia Kuapishwa Rais wa Zimbabwe


HARARE, Zimbabwe

HAFLA ya kuapishwa kwa Rais mteule wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa ambayo ilipangwa kufanyika leo Jumapili jijini hapa, imesitishwa baada ya matokeo kupingwa kisheria mahakamani.

Kiongozi wa MDC, Nelson Chamisa anasema ana ushahidi wa kutosha kuonesha jinsi udanganyifu ulivyofanyika katika uchaguzi huo mkuu wa urais uliofanyika Julai 30.

Chama chake kinasema kura ziliibwa na kufanyia udanganyifu, lakini Kamati ya Uchaguzi inasisitiza kuwa hakukuwa na udanganyifu wowote.

Bwana Mnangagwa alishinda uchaguzi huo kwa kura 50.8% ya kura zote huku Bwana Chamisa akiondoka na asilimia 44.3%.

"Hafla ya kuapishwa kwa rais hakutakuwepo tena kama ilivyopangwa, “alisema Waziri wa Sheria, Ziyambi Ziyambi, baada ya upinzani kuwasilisha pingamizi mahakami Ijumaa.

Katiba ya Zimbabwe inaruhusu mgombea urais kufungua kesi kupinga matokeo ya uchaguzi ndani ya siku saba tangu kutangazwa kwa mshindi wa kiti hicho.

Mahaka ya Kikatiba sasa ina takribani siku 14 kuangalia kesi hiyo ya kupinga matokeo iliyofunguliwa na Chama cha Movement for Democratic Change (MDC).

Chama hicho sasa kinatakiwa kuthibitisha vya kutosha matokeo hayo kuwa hayakuwa halali.

Bwana Chamisa anataka mahakama kumtangaza yeye kuwa ndiye mshindi halali au waite uchaguzi upya, mwanasheria wake aliliambia Shirika la Habari la Uingereza, Reuters.


No comments:

Post a Comment