Na Mwandishi Wetu
UONGOZI wa Viwanja vya Ndege vya Songwe
na Kigoma, umejiandaa kwa kushirikiana na maafisa afya, kuhakikisha hakuna
mgonjwa mwenye dalili za Ebola anaingia nchini, akitokea maeneo ya Tunduma na
nchini Burundi.
Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Songwe,
Bw. Pius Kazeze alimwambia Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege
Tanzania (TAA), Bi.Bahati Mollel kwa njia ya simu kuwa, tayari Maafisa wa Afya
wameshafunga mashine maalum (thermo scanners) inayotambua joto la mwili la
abiria ambaye anasafiri kwa kupitia kiwanja hicho, na likizidi 38 anatakiwa
kutoa taarifa za afya yake.
Bw. Kazeze amesema Kiwanja cha Songwe
ni tofauti kidogo na Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA),
ambapo zaidi wanakagua abiria wanaoondoka kwa kuwa wengi wanatoka mpakani
maeneo ya Tunduma na kwenda maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
“Tayari maafisa Afya wamefunga mashine
ya ukaguzi wa afya eneo la nje la kuondokea abiria kwani kwetu huku tunapata
abiria wengi wanaotoka nchi jirani wanaopitia mpakani Tunduma, hivyo wengi wao
wanatoka nchi zinazopakana na Kongo, ambayo inasadikika ugonjwa wa Ebola umeibuka
kwa kasi kubwa,” alisema Bw. Kazeze.
Hatahivyo, amesema mbali na mashine
hiyo kubwa iliyowekwa sehemu maalum, pia wanamashine mbili ndogo zinazotumiwa
kwa kushikwa mkononi na maafisa Afya, lakini wanakabiliwa na changamoto ya
uhaba wa Watumishi wa afya, ambao tayari wameshaomba kuongezewa mmoja ili
kufanikisha kazi hiyo kuwa rahisi.
Naye Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha
Kigoma, Bw. Theophan Bileha amesema wapo mbioni kiweka kifaa hicho kwa kuwa
wanatarajia abiria kutoka Burundi watakaowasili kwa ndege ya Shirika la Ndege
Tanzania (ATCL), itakayoanza safari zake kuanzia Agosti 30, 2018.
“Tumeshafanya kikao na wenzetu wa Afya,
na wameahidi kuleta mashine mojawapo, tunatarajia abiria wanaotoka Bujumbura,
kwani tumeambiwa ATCL itaanza kwenda huko kuanzia tarehe 30, na hawa wapo
watakaoshuka hapa na wengine wanakwenda kwenye viwanja vingine kulingana na
ratiba ya ndege hii,” alisema Bw. Bileha.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Manispaa
ya Kigoma, Dk. Peter Nsanya amesema mashine hiyo itawekwa kiwanjani hapo kwa
kipindi, ambacho ndege zinatua na baada ya ratiba za ndege kumalizika, wanahamishia
eneo la Bandarini kwa kuwa pia kuna abiria wanaotoka maeneo mbalimbali.
“Sisi tumejipanga kukabiliana na
maradhi haya ikiwa na kuhakikisha hatutaruhusu uingie nchini, na ndio maana
tunaratiba za ndege, ambapo tutakuwa tunakwenda kutoa huduma, na baadaye
kuhamia bandarini,” amesema.
Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Mwanza,
Mohamed Maulid amesema wamejiandaa kwa kushirikiana na Maafisa Afya wamekuwa
wakitumia mashine ya mkono kwa ukaguzi wa abiria wanaotoka nchi za Uganda,
Nairobi na Kongo.
Ugonjwa wa Ebola unaosambazwa kwa virusi
vya Ebola, husababisha homa kali inayoweza kuambatana na kutokwa damu mdomoni,
puani, masikioni, machoni na sehemu nyingine za wazi na unaenea kwa haraka.
Hivi karibuni umetangazwa kutokea nchini
Kongo na kusababisha vifo.
Dalili za Ebola ni pamoja na homa kali,
maumivu ya kichwa na misuli, mwili kulegea, kutapika, kuharisha, vipele na
kutokwa damu.
Juzi Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa
cha Julius Nyerere (JNIA) kilitangaza kuchukua hatua kali za kuweka zuio kwa
abiria wanaongia nchini kupitia Kiwanja hicho, ambapo kumefungwa vifaa ambavyo
vinabaini joto la abiria na endapo litazidi nyuzi joto 38, atatakiwa kutoa
maelezo zaidi ya maisha yake.
Pia abiria wote wanaowasili kwa ndege
zinazotoka nchi jirani na Kongo wanatakiwa kupitia eneo maalum ambalo hutakiwa
kunawa mikono yao kwa dawa maalum ili kuua vijidudu mbalimbali.
No comments:
Post a Comment