Na Mwandishi Wetu, Tanga
MAELFU ya wakazi wa mkoa wa Tanga leo walijitokeza kumsindikiza
katika nyumba yake ya milele msanii mkongwe wa maigizo nchini, Amri Athumani au King Majuto (70) aliyefariki dunia
Jumatano usiku katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa akipatiwa
matibabu.
Majuto alifikishwa Muhimbili June 12 akitokea nchini
India katika hospitali ya Apollo alipokuwa akipatiwa matibabu ya tezi dume, ambapo
alikuwa chini ya uangalizi wa afya yake kabla ya umauti kumkuta.
Majuto ambaye alizaliwa mwaka 1948 alizikwa katika makaburi ya kijijini kwao Kiruku
katika Kata ya Mabokweni jijini hapa.
Katika msiba huo wa kihistoria, Mkuu wa mkoa wa Tanga
Martine Shigella pamoja na mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga Henry Shekifu, waliongoza
mamia ya waombolezaji wakiwemo viongozi wa Serikali na Chama cha Mapinduzi.
Viongozi wengine ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, Mkuu wa wilaya ya Tanga, Thobias
Mwilapwa, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nicholaus
William.
Wengine ni pamoja na viongozi wa dini mbalimbali
nchini.
Katika salamu zake za mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine
Shigella aliwataka wasanii kutokuwa na ubaguzi, wawe na umoja na kuweka
utaratibu wa kumbukumbu za kazi za wasanii waliotangulia mbele za haki.
"Mzee Majuto hakuwa na ubaguzi na kwa upande
wangu alikuwa rafiki yangu mkubwa, wasanii nawaomba muwe na utaratibu wa kuweka
kumbukumbu kwa wasanii waliotangulia mbele za haki," alisema.
Aliongeza: "Tutaendeleza sanaa ya mzee Majuto
iwe kumbukumbu katika maisha yetu na nataka niwahakikishie kuwa mimi binafsi
Martine Shigella na Mkuu wa Mkoa wa Tanga nitatoa ushirikiano katika familia ya
Mzee Majuto watakapohitaji," alisema.
Mbali na viongozi hao pia wasanii mbalimbali wa Bongo
Movies walikuwepo akiwemo, Steve Nyerere, Claud, Mpoki, Wema Sepetu, JB na
wengineo wengi.
Katika kuonesha kuwa jamii ya Watanzania imeguswa na
msiba huo wa msanii huyo nguli na kuonesha mapenzi kila mtu alikuwa akigombea
kubeba jeneza lililobeba mwili wa marehemu wakati linapelekwa msikitini wa
Donge, ambapo ibada ya mazishi iliongozwa na shekh mkuu wa mkoa wa Tanga, Juma
Luwuchu kwa ajili ya kuswaliwa.
HALI
ILIVYOKUWA
Katika msiba huo licha ya wakazi wengi kuhudhuria pia
ilionekana kama baadhi yao walifika kuwashangaa wasanii nyota wa filamu, ambao
wamekuwa wakiwaona katika runinga wakifanya vitu vyao, ambapo walikuwa
wakisukumana ili kuwaona mubashara.
SIKU
YA JUMATANO
Mkoani Tanga wakati mwili wa marehemu Mzee Majuto
unapita katika barabara kuu ya Chalinze-Segera-Tanga ulionekana msafara kuwa ni
mkubwa kutokana na watu wengine kuusimamisha na kutaka kupewa fursa ya kuona
jeneza lake na kusababisha msongamano mkubwa.
Hali hiyo ilisababisha kuchelewesha msafara huo na
kuingia Tanga majira ya saa saba usiku.
Pia nyumba za kulala wageni zilijaa mapema baada ya
watu kutoka mikoa mbalimbali nchini na hata nje ya nchini kufurika Tanga kwa
ajili ya kushiriki msiba wa nguli huyo wa uchekeshaji nchini.
No comments:
Post a Comment