Na Mwandishi Wetu
KLABU ya Michezo ya Uchukuzi (USC) imetakiwa
kubakisha na kuongeza mataji iliyopata katika mashindano yaliyopita ya Mei Mosi
na kutwaa ushindi wa jumla baada ya kujikusanyia vikombe 13.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Ujenzi
na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi), Dk Leonard Chamuriho wakati akifungua
bonanza la kwanza la Sekta ya Uchukuzi lililofanyika katika viwanja vya Makao
Makuu ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Ukonga Banana Jijini Dar es Salaam.
Chamuriho kwanza aliipongeza USC kwa kutwaa ushindi
huo wa jumla wa mashindano ya Mei Mosi yaliyofanyika mjini Iringa mwaka huu,
lakini aliwataka kuulinda ushindi huo na kuongeza vikombe vya michezo mingine,
ambayo hawakutwaa nafasi ya kwanza.
“Nawapongeza Uchukuzi Sports Club kwa kutwaa ubingwa,
lakini kwa kweli kushinda ni jambo rahisi, lakini kuulinda ushindi huo ni jambo
gumu sana, hivyo nawataka muulinde ubingwa huo na muongeze mataji mengine, “alisema
Chamuriho.
Alisema kuwa lazima Uchukuzi waendelee kubaki namba
moja katika michezo, hivyo alisema watafanya kila linalowezekana kuhakikisha
wanaendelea kung’ara katika michezo yote watakayoshiriki.
Mbali na
kuzindua bonanza la kwanza la sekta ya Uchukuzi, pia Chamuriho alizindua rasmi
mazoezi ya USC kwa ajili ya mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara,
Idara na Tawala za Mikoa, Shimiwi, ambayo mwaka huu itafanyika mjini Dodoma
mwaka huu.
Pia aliwasisitizia kuwa atajitahidi kutatua
changamoto zinazoikabili USC ili kuhakikisha klabu hiyo inatekeleza majukumu
yake vizuri ya kuendeleza michezo na kuwawezesha wafanyakazi wa Uchukuzi kuwa
na siha bora.
Katibu Mkuu wa USC, Mbura Tenga wakati akimkaribisha
mgeni rasmi alisema kuwa lengo la bonanza hilo ni kuwakutanisha wafanyakazi wa
wizara bila kujali kada zao, jinsia, rangi au dini.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Ujenzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi), Dk Leonard Chamuriho (mbele) wakati wa bonanza la michezo la Uchukuzi leo. |
Malengo mengine ni kukuza, kusimamia na kuongoza
shughuli za michezo kwa wafanyakazi, kushirikiana na Shimiwi kuendeleza michezo
kwa mujibu wa taratibu zinazojulikana.
Pia kuanzisha na kukuza uhusiano mwema kati ya
viongozi wa wizara, wafanyakazi na wizara zingine huku kubwa zaidi likiwa
kuitangaza Wizara-Sekta ya Uchukuzi kupitia shughuli zake kupitia michezo.
Hivi karibuni USC ilikabidhi makombe 13 ya ushindi wa
Mei Mosi kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, ambapo Mkurugenzi wa
Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta
ya Mawasiliano), Grayson Mwaigombe alipokea vikombe hivyo kwa niaba ya Chamuriho.
Mbali na mazoezi pia kulikuwa na michezo ya kuvuta kamba, mpira wa miguu, mpira wa wavu na mingineyo, ambayo ilichezwa na wafanyakazi wa Sekta ya Uchukizi, ambao walijitokeza kwa wingi leo.
No comments:
Post a Comment