Balozi Maalum wa DStv na moja ya wanariadha
wanaounda timu ya taifa itakayoshiriki mashindano ya riadha ya Dunia mwaka huu
yatakayofanyika mwezi ujao jijini London, Uingereza, Alphonce Simbu, amesema
watanzania watarajie medali kutoka kwa timu hiyo kwani wamejiandaa vizuri.
Akizunngumza wakati wa ziara maalum ya Ofisa Mwandamizi
wa DStv, Johnson Mshana katika kambi hiyo iliyopo Ilboru Arusha ambapo pia
alishuhudia mazoezi ya timu hiyo, Simbu alisema kuwa yeye na wenzake
wamejiandaa kikamilifu kuhakikisha kuwa wanaleta medali nyumbani katika
mashindano hayo makubwa yanayofanyika mapema mwezi ujao.
“Tumejiandaa vizuri na tuna matumaini makubwa
ya kushinda. Tumekuwa tukifanya mazoezi mazito na tuko sawasawa kupambana
katika mashindano hayo, ” alisema Simbu.
Naye Meneja Uhusiano wa Multichoice Tanzania,
Mshana ambayo alitembelea kambi hiyo na kisha kushuhudia mazoezi alisema kampuni
yao imefurahishwa sana na mwenendo wa kambi hiyo pamoja na timu nzima.
“Wakati wote tunapoamua kusaidia katika
maandalizi ya timu tunafahamu fika kuwa timu yoyote bila ya maandalizi ya
kutosha haiwezi kufanya vizuri kwenye mashindano yoyote yale. Hii ndiyo sababu
iliyotusukuma DStv kusaidia katika juhudi hizi za kuiandaa timu yetu ya Taifa
itakayokwenda kuwakilisha nchi katika mashindano ya dunia. Tunataka Watanzania
tushuhudie medali zikija nyumbani.”
Alisema baada ya DStv kuanza kumdhamini Simbu
takriban mwaka mmoja uliopita, wameshuhudia mafanikio makubwa sana, ambayo
yamewatia moyo sana kuongeza nguvu ili kuiimarisha zaidi timu ili hatimaye
iweze kufanya vizuri zaidi na kulikwakilisha vyema taifa kwenye michuano ya
kimataifa.
“Tulianza na Simbu, amefanya vizuri,
ameshinda, sasa tunaongeza wigo wa ushindi kwa timu yetu ya Tanzania na
tunaamini tutashinda, mbali na hayo DStv ilionesha mubashara Mumbai Marathon
tukamuona Simbu akishinda, Tukaonesha Mubashara London Marathon, tukaona Simbu
akivunja rekodi yake, na tutaonesha mubashara Mashindano ya Dunia Mwezi Agosti,
ambapo bila shaka kwa nguvu hii, tutashuhudia tukikwapua medali kedekede na
kuliletea taifa letu sifa kubwa, ” alisema Mshana kwa kujiamini.
Naye Kocha wa timu hiyo Francis John, alisema
kuwa kazi kubwa imefanywa na makocho wanaoinoa timu hiyo hapo kambini na kutokana
na ushirikiano mkubwa kati ya makocha na wachezaji umefanya mazoezi yao kwenda
vizuri.
Alisema wanatarajia kuwa wanariadha hao
watafanya vizuri, kwani hata mmoja wao
aliyekuwa na matatizo ya magoti sasa anaendelea vizuri na bila shaka atashiriki
vizuri kwenye mashindano hayo.
Alisema jumla ya wachezaji saba wakiwemo wanawake watatu na wanaume wanne
watashiriki, ambao ni Failuna Abdi
atashiriki mbio za meta 10,000, Gabriel
Gerald (meta 5,000), huku Magdalena Krispin, Sarah Ramadhani, Said Makula,
Ezekiel Jafar Ng’imba na Alphonce Felix Simbu wenyewe watashiriki mbio za
marathon.
Huku Emmanuel Giniki akiongeza idadi ya
washiriki kwa timu ya Tanzania baada nay eye juzi kufuzu katika mbio za meta
5,000 baada ya kufanya vizuri katika mbio za kimataifa nchini Ubelgiji.
Giniki alimaliza katika nafasi ya saba kwa
kutumia dakika 13:13:24 na kuongeza idadi ya washiriki wa Tanzania kufikia
wanariadha nane.
Aidha, timu hiyo ya taifa ya Tanzania
inatarajia kukabidhiwa bendera Julai 31 katika Hoteli ya Kilimanjaro jijini Dar
es Salaam tayari kushiriki mashindano hayo ya dunia yatakayoanza Agosti 3 hadi
15.
No comments:
Post a Comment